Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, kukomesha mara moja wizi wa mifugo unaofanywa wilayani humo ikiwemo katika Ranchi ya Mzeri ili wafugaji waweze kunufaika na uwekezaji wao.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (12.08.2021) alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika ranchi hiyo iliyo chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kusikitishwa na kitendo cha wizi wa mifugo kilicholalamikiwa na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo.
Mhe. Ulega amemtaka Kamanda wa Polisi Wilaya ya Handeni kuhakikisha anakomesha vitendo hivyo vya wizi na endapo mhusika akifikishwa mahakamani basi mahakama ina utaratibu wake wa kuhakikisha haki inatendeka katika kukomesha vitendo hivyo.
“Nimefarijika sana OCD aliponiambia nataka nikuambie Naibu Waziri hapa mimi nipo katika kusimamia haki vituo vyote ambavyo kesi na malalamiko yamekuwa mengi amesema atasimamia vyema malalamiko yote yakiwemo ya watu wanaofanya vitendo hivyo kuendelea kufanya licha ya kuchukuliwa hatua za kisheria.” Amesema Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa wizara inataka kuona wizi wa mifugo unakomeshwa mara moja na kwamba jambo hilo lazima lisimamiwe vyema.
Awali baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika Ranchi ya Mzeri wamemfahamisha Naibu Waziri Ulega kero ya wizi wa mifugo hali inayowafanya kushindwa kutimiza malengo yao ya uwekezaji pamoja na kukosekana kwa mahusiano mema kati ya wawekezaji na wakazi wa maeneo hayo.
Social Plugin