Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
Zaidi ya nyumba 19 zimeteketea kwa moto katika kitongoji cha Shaurimoyo kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara ,Rufiji ,Pwani mara baada ya mwananchi mmoja akiwa anasafisha eneo lake kwa moto ndipo ulimshinda na kuteketeza nyumba zipatazo 19 za wananchi pamoja na mali na thamani zilizopo ndani ya nyumba hizo .
Aidha hakuna majeruhi yoyote katika ajali hiyo wala kifo.
Kufuatia janga hilo ,Mkuu wa mkoa wa Pwani Aboubakari Kunenge pamoja na wajumbe wa kamati ya usalama ya wilaya ya Rufiji wamefika kwenye tukio la moto lililotokea usiku wa kuamkia agost 30 mwaka huu, ili kuona athari iliyotokea na jitihada ambazo uongozi wa wilaya wamezichukua kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.
Kunenge alitoa pole kwa serikali ya wilaya pamoja na wananchi waliokutwa na madhira hayo na kuwapongeza wakazi wa maeneo ya karibu kuweza kuwapatia hifadhi wananchi wenzao waliokutwa na ajali hiyo .
Aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo kufanya haraka kujua tathmini ya athari iliyopatikana ili kuweza kuwasaidia waliopata ajali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele ,alieleza kama wilaya hatua walizochukua baada ya kutokea tukio hilo .
Alitoa rai kwa wakazi wa wilaya hiyo kuwa makini wakati wanachoma moto kwani kwa sasa ni kipindi cha upepo mkali.
Wananchi wa eneo hilo nao wameeleza tukio jinsi lilivyowaathiri hivyo kuomba serikali kuweza kuwasaidia kwa haraka maana hawana mahala pakuishi.
Social Plugin