Maafisa wa polisi wanachunguza kisa kimoja ambapo mwenzao kutoka kituo cha Polisi cha Njoro nchini Kenya amepiga risasi na kumuua mpenzi wake kabla ya kujigeuzia bunduki na kujiua.
Konstebo Bernard Sivo alimpiga risasi na kumuua Mary Nyambura katika Hospitali ya kaunti ndogo ya Njoro alimokuwa amekwenda kutafuta matibabu baada ya kuvunjika mguu.
Kulingana na ripoti ya polisi, imebainisha kuwa wanandoa hao awali walipigana nyumbani kwao na kumchochea Sivo mwenye umri wa miaka 28, kumpiga Nyambura na kumvunja mguu wake wa kulia.
Nyambura, 29, alifaulu kwenda hospitalini na ni katika harakati ya kupokea matibabu ndipo afisa huyo alitokea akiwa amejihami na bunduki aina ya AK-47.
Kisha Sivo, alimfyatulia Nyambura risasi kadhaa na kumuua papo hapo. Hii iliwachochea madaktari ambao walikuwa wanamshughulika kukimbilia usalama wao.
Kisha afisa huyo alirejea kazini akiwa na hasira za mkizi na kuonekana akifyatua risasi kiholela kituoni humo na kuhatarisha maisha ya maafisa wenzake.
Maafisa waliitwa kushirikiana kumpokonya bunduki lakini kwa bahati mbaya alijipiga risasi ya shavu iliyotokea kichwani na kumuua papo hapo.
Katika eneo la tukio, polisi walipata bunduki aina ya AK 47 na risasi 11. Mwili wa marehemu Nyambura ulipatikana ukiwa na majeraha ya risasi kwenye mkono wake wa kulia na upande wa kulia wa mgongo wake.
Miili ya wanandoa hao ilipelekwa katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Egerton ikisubiri kufanyiwa upasuaji wa maiti.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin