POLISI MOROGORO YADAKA WATUHUMIWA KIBAO



Na Jackline Lolah Minja - Morogoro
Jeshi la polisi mkoani Morogoro linawashikilia watuhumiwa 16 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kusafirisha bangi, wizi wa mali inayosafirishwa, mali za serikali pamoja matumizi ya silaha kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24 ,2021 Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro SACP  Fortunatus Muslim amesema mnamo tarehe 22/7/2021 saa saba usiku maeneo ya Juniour Seminary wamefanikiwa kumkamata Omari Idd (36) mkazi wa Chamwino akiwa na tv mbili flat screen aina ya boss inchi 55 na LG nchi 60 pamoja na laptop 6 za aina mbalimbali.

"Huyu Omary Idd licha ya vitu hivyo lakini pia tulifanikiwa kumkuta na viatu yeboyebo pair 5, viatu vya kike , masweta ya shule aina ya MAC ,mafuta ya mgando dozeni 19 na nguo mbalimbali za jeans ambazo zinadaiwa kushushwa kwenye magari barabara kuu", alisema Muslim.

Katika hatua nyingine jeshi hilo la polisi limefanikiwa kuwashikilia watu saba akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wilaya ya Gairo, maafisa ugavi  wanne na madereva wa tatu  kwa tuhuma za wizi wa mabati 1172.

"Mnamo tarehe 17 june majira ya saa nane mchana maeneo ya ujenzi kata ya mbumi wilaya ya Kilosa ulitokea wizi wa mabati ambayo ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Kilosa yaliyohifadhiwa kwenye stoo na wizi huo umefanyika bila kuvunja makufuli wala milango na  watuhumiwa hao bado wanahojiwa na upelelezi unaendelea wakikutwa na hatia watafikishwa mahakamani",alisema Muslim.

Kamanda Muslimu amewasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wageni wanaoingia mkoani hapo kuwa watulivu kwa kuwa jeshi hilo halitamvumilia yoyote atakayevunja sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post