Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AZUNGUMZIA KESI YA FREEMAN MBOWE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA anayekabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na ugaidi, kesi yake hiyo ilikuwa imefunguliwa  tangu Septemba mwaka 2020 lakini uchunguzi ulikuwa bado unafanyika dhidi yake.

Amesema kwa wenzake kesi zao zilishaanza kusikilizwa, lakini Mbowe upelelezi wake ulikuwa haujaisha.

Rais Samia alieleza hayo  kwa mara kwanza jana katika mahojiano na Shirika la Utangaza la Uingereza (BBC), yaliyoongozwa na mtangazaji mwandamizi wa kituo hicho, Salim Kikeke kutoka Ikulu, Dar es Salaam.

“Tumeingia kwenye uchaguzi, tumemaliza. Sasa polisi wamemaliza uchunguzi wao wamemhitaji kwa ajili ya kuendelea na kazi yao. Lakini kama utakumbuka Mbowe hakuwa nchini kwa kipindi kirefu, alikuwa Nairobi.

“Lakini alivyoingia nchini aliitisha maandamano ya Katiba. Nadhani yalikuwa na mahesabu akijua kuwa ana kesi ya namna hiyo na hii vurugu anayoianzisha, akikamatwa aseme kwa sababu ya Katiba,” alieleza Rais Samia.

Samia alisema suala la Mbowe lipo mahakamani hana uhuru wa kulizungumzia kwa kina, huku akishauri jambo hilo liachwe katika chombo hicho cha kutenda haki ili kifanye kazi yake na kuuonyesha ulimwengu kama shutuma za Mbowe za kweli au la.

Kuhusu kukutana na viongozi wa vyama siasa, Rais Samia amesema; “Nilitaka kukutana nao, lakini si wakiwa wamechambukachambuka, kwa sababu hawa wana vyama vyao vidogo vidogo na mabaraza yao. Nilitaka kwanza wajiunde kwenye baraza lao ambalo lilifanya uchaguzi wiki chache zilizopita.”

Amesema kwa vile wameshafanya uchaguzi na kamati zao ndogo zimejiunda vizuri, atatafuta siku ya kuzungumza nao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com