Rais mpya wa Zambia Hakainde Hichilema Jumapili ameteua wakuu wapya wa jeshi na kuwaondoa wakuu wote wa polisi huku akiahidi kumaliza utawala kandamizi wa mtangulizi wake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, makundi ya kutetea haki za binadamu yamemlaumu mtangulizi wa Hichilema, Edgar Lungu kwa kuongoza msako mkali dhidi ya raia pamoja na ukatili wa polisi ambao wamelaumiwa kuua takriban watu watano tangu alipochaguliwa mwaka 2016.
Hichilema aliyechukua madaraka wiki iliyopita amewahi kukamatwa mara nyingi katika maisha yake ya kisiasa na utawala uliopita. Kupitia televisheni ya taifa Jumapili, Hichilema alitangaza wakuu wapya wa jeshi pamoja na wale wa jeshi la anga.
Wakati huo huo alitangaza kusimamishwa kazi mara moja kwa makamishna wote bila kutoa maelezo zaidi. Pia amewataka polisi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuwazuia washukiwa.
Tags:
habari