Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA BURUNDI YAPEWA ENEO LA KUJENGA BANDARI KAVU TANZANIA


Serikali ya Burundi imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia enao la hekta kumi kwa ajili ya kujenga Bandari kavu eneo la Kwala, mkoani Pwani.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Burundi nchini Tanzania  Bw. Gervais Abayeho, wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha Balozi huyo pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.

Aidha, Balozi Abayeho,  ameongeza kuwa kupatikana kwa eneo hilo kutasaidia  wafanyabishara wa Burundi kuweza kuhifadhi shehena zao kabla ya kusafirisha kwenda  Burundi , na hivyo kusaidia kupunguza gharama za utunzaji wa mizigo yao wanazozipata kwa sasa.

“Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kutupatia eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu, tunaamini upatikanaji wake utakuwa mkombozi kwa wasafirishaji wetu”, amesema Balozi Abayeho.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt.Leonard Chamuriho, amemhakikishia Balozi huyo pamoja na Ujumbe aliokuja nao kutoka nchini Burundi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaama na kupeleka nhini humo.

Chamuriho amefafanua kuwa kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuboreshwa hivyo ufanisi umeongezeka   wa kuhudumia mizigo inayoingia na kutoka Bandarini hapo.

Waziri ameongeza kuwa  hatua  ya serikali kuipa Serikali ya Burundi eneo la kujenga Bandari kavu ni jambo jema ambalo linapelekea kujenga mahusiano mema baina ya nchi hizo mbili.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire,  amesema kuwa pamoja na Balozi huyo na ujumbe wake, kutembelea  Bandari na Reli ya kisasa pia wamesaini kwa pamoja na wajumbe wa Tanzania makubaliano ya awali ya kuwakabidhi eneo la ujenzi wa Bandari Kavu.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania  nchini Burundi Dkt. Jilly Maleko, amesema kuwa  upatikanaji wa eneo hilo la Bandari kavu kutapelekea wafanyabiashara wa Burundi  kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa kiwango kikubwa.

Ujumbe zaidi ya watu kumi kutoka nchini Burundi ulipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelzwa na Wizara hiyo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na Bandari ya Dar es salaam na Kigoma

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com