Serikali imekusanya zaidi ya Sh.48 bilioni, kupitia tozo ya miamala ya simu .
Hayo yameelezwa leo Ijumaa, tarehe 20 Agosti 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akitoa kauli ya Serikali juu ya hatua ambayo imefikia kuhusu marekebisho ya tozo ya miamala ya simu, jijini Dar es Salaam.
Amesema kati ya fedha hizo, zilizokusanywa kupitia tozo ya miamala ya simu iliyoanza tarehe 15 Julai 2021, ni Sh. 48.4 bilioni. Huku Sh. 28 bilioni ikitoka katika tozo ya mafuta.
Dk. Mwigulu amesema, Serikali imepeleka Sh. 22 bilioni, katika Wizara Ofisi ya Rais-Tamisemi, kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.
“Upande wa tozo ya mafuta mwezi ulipita wa Julai, ambayo na yenyewe mpaka wiki ijayo Tamsiemi watakuwa wamepokea Sh. 24 bilioni, hizo ni mahusi kwa ajili ya barabara za vijijini. Kutoka tarehe 1 Agosti 2021, tutakuwa na zaidi ya Sh. 20 bilioni nyingine na kuendelea,” amesema Dk. Mwigulu.
“Tumeona ni vema kuhabarisha umma kuhusu tozo, ombi langu moja ni hili jambo ni letu sote, si la serikali. Kila mtanzania ulipo, lazima utambue nchi ni yako na pesa ni yako hapo ulipo na haya tunataka kufanya ni yako, sisi tunaofanya ni dhamana tu,” amesema.
“Kuanzia mwaka kesho tutaanza kupokea kidato cha tano ambao wametokana na sera ya elimu bila malipo, tunafahamu mahitaji yatakuwa ni makubwa. Tunaona kabisa mambo haya tunapaswa kuyafanyia kazi na si kuyaahirisha.
“Bado yapo maeneo nchini ili uweze kufika kwenye kituo cha afya inakulazimu uende ama kwenye kata nyingine au tarafa nyingine, kwa umuhimu wa jambo hili tukasema sio la kuacha bila kufanyia kazi.
“Hapa katikati kuliibuka maneno mengi sana na ilielezwa kwamba shughuli za miala ilipungua, niseme kwamba Watanzania waliendelea kutumiana na shughuli za kufanya miamala hazikuathirika na takwimu ziko pale pale.
“Sisi Wizara ya Fedha na Mipango tunaamini kwamba, tunapopeleka Bil 48 kwenye uchumi maana yake tunaongeza kasi ya kutumiana fedha na kuifanya fedha iende kwenye mzunguko na kasi ya kubadilisha fedha kwenye mikono itaongezeka pia.
“Katika suala la tozo za miamala ya simu kwa sasa, kuna gharama za mtoa huduma na gharama zilizowekwa na serikali, lakini jumla yake yote anabeba mwananchi.
“Tukaangalia hili suala la tozo za miamala ya simu, tukasema tuangalie namna ya kwamba serikali na watoa huduma tukae kwa pamoja tuone namna gani tutampunguzia gharama ya jumla kwa mwananchi. Tupo katika hatua ya mwisho katika hili."- Dr. Mwigulu