Na Abby Nkungu, Singida
HALMASHAURI za mkoa wa Singida zimeanza kutenga bajeti ya fedha kila mwaka kwa ajili ya kufuatilia na kuratibu masuala ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kuhakikisha kizazi hicho kinalindwa, kutunzwa na kustawi kama ilivyo kwa makundi mengine.
Hayo yalibainishwa na Ofisa lishe wa mkoa wa Singida, Teda Sinde katika mahojiano maalum wakati wa Maadhimimsho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani yaliyofanyika hivi karibuni.
Alisema kuwa miongoni mwa mikakati ya mkoa katika kuhakikisha kizazi hicho kinaendelea kulindwa, kutunzwa na kustawi ni kwa kila halmashauri kutenga shilingi 1,000 kwenye bajeti yake ya ndani kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano ili kufuatilia masuala ya lishe.
Sinde alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri huo wanapata lishe bora kulingana na mazingira ili kuimarisha ulinzi, usalama na ustawi wa kizazi hicho muhimu kwa Taifa letu la baadae.
Alieleza kuwa pamoja na kutenga fedha, mikakati mingine ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto katika vituo vya kutolea huduma za afya, kutumia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wanasema kuwa licha ya juhudi hizo za Serikali bado kuna changamoto ya mila potofu ambapo jamii nyingine zinazuia wajawazito au watoto kula baadhi ya vyakula vyenye virutubisho muhimu.
Mtafiti wa masuala ya Mila ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Mstaafu, Patrick Mdachi
alisema kuwa katika baadhi ya makabila watoto na wajawazito kula mayai au maini ni mwiko kwao suala ambalo kihalisia linaathiri lishe bora.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Ofisa miradi wa Shirika la World Vision Tanzania linalotekekeza mradi wa lishe kwa mikoa ya Singida na Shinyanga, Mwivano Malimbwi ambaye alisema elimu juu ya masuala ya lishe bado ni muhimu katika jamii ili kuhakikisha kizazi cha watoto kinakuwa na kustawi vyema.
Takwimu za kidunia zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 7.7 ya watu wote duniani ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wakati mkoani Singida, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kulikuwa na watu milioni 1.5 kati yao 350,000 ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambayo ni sawa na asilimia 23.3 tu.
Social Plugin