TAFIRI YATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA KWA WAVUVI WADOGO

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), (hawapo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na kuwataka wafanye tafiti zenye tija kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo juu ya zana za uvuvi na teknolojia ya kisasa ya kufahamu maeneo yenye samaki. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akitoa taarifa fupi kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), mara baada ya kufika katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, ambapo ameelezea changamoto za kifedha zinavyowarudisha nyuma katika kufanya tafiti. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

 


Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), mara baada ya Naibu Waziri Ulega kumaliza ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaaam. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

 

 

 

Na. Edward Kondela

 

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kujikita kwenye tafiti zenye tija kwa wavuvi wadogo na kushauri vyema kwenye mamlaka za serikali juu ya njia mbalimbali zikiwemo za kiteknolojia ili sekta ya uvuvi iwe na tija zadi kwa mvuvi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (10.08.2021) Mkoani Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kujionea namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

 

Akiwa katika ofisi za TAFIRI zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Ulega amefafanua kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo ni lazima zijibu changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo hivyo ni muhimu kufikiria mambo ya kufanywa ili kuondoa changamoto hizo ikiwemo ya zana za uvuvi kutokana na mazingira ya sasa.

 

“Nyie ni wataalam wasomi lakini msiache kuwashirikisha na kuwasikiliza wavuvi ambao wamekuwa wakishinda baharini muda mrefu zaidi, mna mambo ya kujifunza kutoka kwao ili kuhakikisha mnawawekea mazingira bora ya kufanyia shughuli zao, ikiwemo kuhakikisha hawavui samaki kwa kuvizia bali wawe wanaelekezwa maeneo yenye samaki kwa kutumia teknolojia ya kisasa.” Amesema Mhe. Ulega

 

Aidha, ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezeko la watu na mahitahi ya samaki, TAFIRI inapaswa kufikiria kwa kina zaidi kwa kufanya tafiti nyingi zaidi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI), namna ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania hususan wadau wa sekta ya uvuvi wananufaika kupitia tafiti zenye matokeo chanya kwao.

 

Amesema ubunifu pekee ndiyo unaweza kuifanya TAFIRI kuwa karibu zaidi na wavuvi kwa kuwa watakuwa wanapata mafanikio kupitia uvuvi kwa tafiti ambazo zitawapatia zana sahihi za uvuvi kulingana na mazingira ya sasa pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kufahamu maeneo yenye samaki badala ya kuvua samaki kwa kuvizia maeneo ambayo hawana taarifa za uhakika juu ya uwepo wa samaki pamoja na majira yake.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amemuarifu Mhe. Ulega kuwa taaisisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hali inayosababisha kushindwa kufikia baadhi ya malengo waliyojiwekea katika tafiti kutokana na ukosefu wa vifaa vikiwemo vya maabara.

 

Pia, Dkt. Kimirei amesema licha ya changamoto hizo TAFIRI imekuwa ikiendelea kuhakikisha inafanya tafiti ambazo ni muhimu kwa sekta ya uvuvi ili kuwa na taarifa sahihi juu ya sekta hiyo ili taifa liwe na dira ya kufahamu rasilimali za uvuvi zilizopo katika Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo hapa nchini na kufahamu njia sahihi za kutunza rasilimali hizo na pia kuhakikisha zinawanufaisha wavuvi.

 

Nao baadhi ya watumishi wa TAFIRI wamemuomba Naibu Waziri Ulega, kuwasaidia kupatikana kwa meli maalum kwa ajili ya utafiti kwa kuwa wanashindwa kwenda baharini kufanya tafiti kutokana na ukosefu wa meli ya aina hiyo, jambo ambalo Mhe. Ulega amesema atalifanyia kazi ili taasisi hiyo iweze kupata meli na kufanya tafiti mara kwa mara, pamoja na kupata magari ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post