Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Njedengwa jijini Dodoma leo Tarehe 27 Agosti, 2021.
***********
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwepo kwa
nafasi mbili za Ubunge katika majimbo ya Konde mkoa wa Kaskazini Pemba na
Ushetu mkoani Shinyanga.
Akizungumza na Vyombo vya habari leo tarehe 27
Agosti 2021, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson
Mahera amesema uchaguzi huo mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Oktoba 9,2021.
“Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo
la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Jimbo la Ushetu Wilaya
ya Ushetu mkoani Shinyanga ipo tayari,”alisema Dkt. Mahera.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea
barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Kumb.
Na. CEA.137/400/02/111 ya tarehe 16 Agosti 2021, akiitaarifu kuhusu kuwepo kwa
nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga.
Nafasi hiyo inatokana na kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo hilo, Elias John Kwandikwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dkt Mahera amesema taarifa hiyo ya Spika ni
kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Aidha, kwa upande wa Jimbo la Konde, Dk
Mahera amesema mnamo tarehe 2 Agosti, 2021 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa
taarifa kwa umma kuhusu kuwepo wazi kwa
Jimbo la Konde lilipo katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba
kutokana na mbunge mteule wa jimbo hilo,
Sheha Mpemba Faki kujiuzulu.
“Tume ilipokea barua yenye Kumb. Na.
CMM/T.40/Vol.I/72 ya tarehe 2 Agosti, 2021 kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ikitoa taarifa kuwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde, ameandika
barua, kueleza kwamba hakuwa tayari kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Konde
kutokana na changamoto za kifamilia,”alisema Dkt. Mahera na kuongeza kuwa kutokana
na hatua hiyo, Tume ililitangaza jimbo hilo kuwa wazi kwa kuwa Mbunge huyo
Mteule alikuwa bado hajatangazwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa
kifungu cha 81(c) (iii) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Awali mnamo tarehe 18 Julai, 2021 Tume
iliendesha Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Konde kujaza nafasi iliyoachwa wazi
kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Khatibu Saidi Haji kupitia
chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT –WAZALENDO)
Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo
yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza Septemba
13 hadi 19,2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo
ukifanyika Septemba 19 mwaka huu.
Aidha, Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi
katika majimbo hayo ya Ushetu na Konde utaanza Septemba 20, 2021 na zitafikia
ukomo wake Oktoba 8 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 9 Oktoba ,2021.
Dk Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria,
kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na
Tume katika kipindi cha Uchaguzi mdogo.