UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NI ZAO LA UTAWALA BORA

 

Mei 3 kila mwaka jamii ya ulimwengu huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari tangu Umoja wa Mataifa ulipoidhinisha siku hiyo. Lengo la siku hiyo ni kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kuzikumbusha serikali umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza kama inavyolindwa katika Ibara ya 19 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu.

Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa watu haki yao ya kupata na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia. Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni chachu katika kukuza misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kwani husaidia raia na serikali zao kupokea na kutoa taarifa au maoni kuhusu mambo yanaoathiri maisha yao ya kila siku.

Katika kuangazia hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini, tujikumbushe uchambuzi wa hali halisi kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu 2019 kwa jambo ambalo liliakisi matukio  yaliyotishia na kudidimiza uhuru wa vyombo vya habari sambamba na haki ya kupata taarifa, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni. Mambo makuu yanayoathiri uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania ni pamoja na ;

Uwepo wa Sheria Kandamizi kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari; Sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na ufurahiaji wa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania. Mwezi Machi 2019, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ilitoa hukumu yake kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, kufuatia kesi iliyofunguliwa na LHRC, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Katika hukumu hiyo, Mahakama ilithibitisha vifungu vya 7(3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j); vifungu vya 19,20 na 21; vifungu vya 35,36,37,38,39 na 40; vifungu vya 50 na 54; vifungu vya 52 na 53; na vifungu vya 58 na 59 kuwa vinakiuka haki ya uhuru wa kujieleza na Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Vile vile katika kupigania mazingira rafiki kwa vyombo vya habari nchini, watu binafsi mashiriki na taasisi ikiwemo MISA nguvu na maarifa makubwa yameendelea kuwekezwa ili kuhakikisha siku moja uwanja wa habari na taarifa unakuwa huru zaidi ya sasa.

Sheria nyingine ambazo ziliendelea kuminya uhuru wa kujieleza kupitia baadhi ya vifungu vyake ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji Habari ya mwaka 2016, na Kanuni za Maudhui ya Mtandao. Sheria hizi zinajumuisha vifungu ambavyo havikidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Uwepo na utekelezaji wa sheria hizi uliendelea kuchangia upunguaji wa nafasi ya ushiriki wa wananchi kwa mwaka 2019.

Adhabu Kali kwa Vyombo vya Habari; vyombo vya habari vimekuwa wahanga  wa kupewa adhabu ya kufungiwa na kulipa faini kwa madai ya kukiuka Kanuni za Maudhui ya Mtandao, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutoendana na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Vyombo hivyo vya habari ni Gazeti la The Citizen, na televisheni za mtandaoni za Kwanza Online TV, Watetezi TV na Ayo TV.

Mara nyingi makosa yanayotumika kuvifungia na kuvipiga faini kubwa vyombo vya habari yamekuwa ni makossa ambayo yangeweza kurekebishwa na vyombo hivyo kuendelea na utendaji bila kufungiwa.

Mbali na juhudi zote hizi ikumbukwe itakuwa ni kazi bure kama waandishi hawatazingatia maadili, sheria na taratibu zinazowangoza kwani huu ndio msingi wa kuwa na uwiyano katika kuihudumia jamii na kuepuka misuguano.

Mathalan Serikali inastahili pongezi kwa kutoa mwanya na nafasi kwa taasisi hizi kupaza sauti kwaajili ya uhuru wa vyombo vya habari lakini bila ya kusahau Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alitangaza msimamo wake juu ya kushirikiana na vyombo vya habari sambamba na kufungua milango aliagiza vyombo husika ikiwemo idara ya Maelezo kuachana na taratibu ya fungia-fungia vyombo vya habari kwa kasi bali kasi hiyo ielekezwe kwenye kuvilea ili visimame katika misingi ya sheria.

"Nasikia kuna vyombo vya habari vilivyofungiwa fungiwa na TV za mikono, vifungulieni na vifuate sheria na muongozo wa serikali" alinukuliwa Rais Samia.

Ni dhahiri kuwa Rais Samia amerejesha tumaini na kuuwasha mshumaa wa amani katika mioyo ya wanahabari na sasa watachapa kazi kwa bidii zaidi ndio maana narejea tena kusema uhuru wa vyombo vya habari katika nchi yeyote ile unachagizwa na utawala bora wa serikali inayotawala.

Ingawa baadhi ya sheria zilizopigiwa kelele kuwa zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari bado zingalipo nchini lakini kwa kauli za Rais Samia, huu ni mwelekeo mzuri katika kuelekea uhuru wa vyombo vya habari nchini wito wangu kwa wanahabari wote ni kutenda kwa haki na kuishi kwa kufuata na kuzingatia maadili ya taaluma.

'YAJAYO YANAFURAHISHA"

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post