Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ULEGA ABAINISHA MIKAKATI YA KUBORESHA MNADA WA PUGU

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ngw’ilabuzu Ludigija (mwenye kaunda suti) juu ya maboresho ya miundombinu inayofanywa katika mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Miundombinu na Uendelezaji Masoko ya Mifugo Bw. Humphrey Killo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akikagua ubora wa matofali yanayotumika katika ujenzi wa uzio katika mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika mnada huo ili kusikiliza kero zinzowakabili wafanyabiashara na kukagua maboresho ya miundombinu.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akisikiliza maelezo mbalimbali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ngw’ilabuzu Ludigija (mwenye kaunda suti) na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Miundombinu na Uendelezaji Masoko ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Humphrey Killo, Mhe. Ulega amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Ilala, mnada wa kimataifa wa Pugu na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, baada ya kukagua eneo la kuhifadhia mbuzi katika mnada huo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja.

 

Na. Edward Kondela

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesikiliza kero za wafanyabiashara wa mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam ukiwemo utaratibu wa utoaji wa huduma katika mnada huo, uhaba wa maji, uchakavu wa miundombinu ya kuhifadhia mifugo na ubovu wa eneo la kushusha na kupakia mifugo.

 

Akiwa jijini Dar es Salaam katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mnada huo (26.08.2021), Naibu Waziri Ulega amearifiwa pia changamoto ya ukosefu wa taa ndani ya mnada huo, jambo ambalo Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Bi. Tabu Shaibu ameahidi kulishughulikia ndani ya wiki moja.

 

Wakifafanua juu ya changamoto hizo baadhi ya wafanyabiashara hao wamemueleza Naibu Waziri Ulega kuwa biashara katika mnada huo inaanza saa moja asubuhi, lakini changamoto wanayoipata ni suala la ukatishaji wa ushuru ambapo watumishi wanafungua ofisi saa tatu asubuhi kwa mujibu wa mwongozo wa minida.

 

Aidha wameeleza kuwa bado wanakabiliana na kero mbalimbali ikiwemo ya uchakavu wa paa la eneo la kuhifadhia mifugo yao, wakisema wakati wa mvua wanapata shida ya kujikinga wao pamoja na mifugo wanayoihifadhi.

 

Akifafanua juu ya utatuzi wa kero hizo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amewaelekeza watendaji wa mifugo wa wizara hiyo, kurekebisha mwongozo wa mnada ili kuruhusu shughuli za huduma kuanza saa moja asubuhi badala ya saa tatu asubuhi.

 

“Lengo la ziara hii ni kuangalia utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo kukagua ujenzi wa uzio unaozunguka mnada huu pamoja na kupokea na kushughulikia kero zinazowakabili wafanyabiashara.” Amesema Mhe. Ulega

 

Ameongeza kuwa mwongozo huo uliwekwa wa saa tatu asubuhi kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaweza kufanya ujanja wa kwenda na mifugo katika minada kisha kuondoka nayo kwa kisingizio cha kukosa wateja na kuikosesha serikali mapato.

 

Amebainisha sababu nyingine kuwa ni upatikanaji wa huduma za kifedha kwa muda wa kuanzia saa moja asubuhi, hata hivyo amesema kitendo cha huduma hizo kuanza saa tatu badala ya saa moja asubuhi kinasababisha watanzania kukosa biashara kwa wale wanaotegemea mazao ya mifugo.

 

“Shusheni muda hadi saa moja asubuhi, ongeeni na watu wa mabenki waanze kutoa huduma kuanzia muda huo. Polisi wapo wana uwezo na uweledi wataimarisha ulinzi. Rais Samia Suluhu Hassan anapenda watu wafanye kazi na kulipa ushuru naagiza shusheni muda.” Amesema Mhe. Ulega.

 

Kuhusu changamoto la paa, Mhe. Ulega amesema mkandarasi ameshapatikana na kazi ya kupaua na kurekebisha eneo itaanza mara moja  na itafanyika usiku na mchana na kwamba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeshafikisha maji katika mnada huo.

 

Ameongeza kuwa kilichobaki ni miundombinu ya mabomba na mchakato utakamilika ndani ya wiki moja na kuhusu uzio kazi imeshaanza na amemuelekeza mkandarasi akamilishe kazi hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu.

 

Pia Naibu Waziri Ulega amewaarifu wafanyabiashara hao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameupa mnada wa Pugu Shilingi Milioni 600, kwa ajili kutengeneza eneo la kunyweshea mifugo maji na mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kazi hiyo itakayoanza wiki ijayo.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com