Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha wanasimamia haki na amani na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (12.08.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kuibainisha hayoa kwenye kikao chake na uongozi wa wilaya hiyo na kuwataka pia wataalam wa sekta ya mifugo washirikiane vyema na viongozi katika kutoa pia elimu juu ya umuhimu wa makundi hayo mawili ya wakulima na wafugaji.
Mhe. Ulega amesema wafugaji lazima waishi kwa upendo maeneo walipo pamoja na wafugaji wengine na wakulima kwa kuwa ni dhambi kubwa kuchukua mifugo na kuingiza kwa makusudi kwenye shamba la mkulima.
“Kitendo cha ng’ombe kupelekwa kwenye mashamba ni jinai kama jinai nyingine siyo haki kwa mkulima au mfugaji kuchukua hatua kinyume na taratibu na viongozi wa kijiji wawe wasimamizi wa haki na amani na wasifanye upendeleo pamoja na kufanya vitendo vyovyote vya rushwa.” amesema Mhe. Ulega
Naibu Waziri Ulega amelazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa Wilaya ya Handeni kuwa kumejitokeza migogoro baina ya wakulima na wafugaji hadi kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu ya mahusiano baina ya makundi hayo mawili.
Katika taarifa hiyo wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inaweka mikakati mbalimbali ya kukomesha migogoro hiyo ambayo imekuwa ikisababisha hofu, ukizingatia Wilaya ya Handeni ina mifugo mingi na imekuwa ikifanya biashara ya kupeleka mifugo ndani na nje ya nchi.