Kaka wawili na binamu wao wawili wameuawa kinyama siku ya Jumapili, Agosti 8,2021 mtaani Kitengela kaunti ya Kajiado nchini Kenya na wakazi waliodhani walikuwa wezi wa mifugo.
Fred Mureithi, 30 kakake mdogo Victor Mwango, 25, na binamu wao Mike George , 29 na Ncholas Musa, 28 walikuwa wamemtembelea jamaa wao mtaani Kitengela kabla ya kukumbana mauti.
Kwa mujibu wa taarifa za The Star, wanne hao walikuwa washerehekee birthday ya Victor Mwangi ambaye alikuwa anatimiza umri wa miaka 25 siku hiyo.
Ilipofika mwendo wa saa kumi na mbili jioni, wanne hao waliondoka wakiwa na pikipiki tatu kwenda kutafuta kuku eneo la Kisaju ambayo wangepika jioni hiyo.
Walipofika katika eneo la Enkamulyat karibu na mto waliegesha piki piki zao, inasemekana moja iliharibika, katika harakati za kuitengeneza, hapo ndipo wakazi waliitana wakidhani ni wezi wa mifugo.
Bila huruma , wakazi wanasemekana kuwashambulia kwa mikuki wanne hao na kuwaua papo hapo.
Imeripotiwa kuwa eneo hilo limekuwa likishuhudia sana visa vya wizi wa mifugo na ndiyo huenda wakazi walichukua sheria mikononi.
Kulingana na marafiki wao waliozungumza na wanahabari, wanne hao walikuwa wameenda kwa nyumba mpya ya dadake George ambapo wangefanyia sherehe ya Victor pamoja na ya kuingiza nyumba.
Rafiki yao aliyetambulika kwa majina Francis Ndegwa, alisema wanne hao waliafikiana wale kuku kwa ugali kama sapa, kwa kuwa haikuwa, waliamua kutoka wote kwenda kununua lakini kumbe ilikuwa siku yao ya mwisho hapa duniani.
"Wale waliowavamia walikuwa wanachama wa nyumba kumi eneo la Kitengela, waliwashuku kwa kuwa wezi wa mifugo, kila mmoja wao alikuwa na jeraha la mkuki kwenye kichwa,"Ndegwa alisema.
Imeripotiwa kuwa, washambuliaji pia walichoma piki piki zao na vitambulisho vya wanne hao.
Kulingana na Ndegwa mamake Victor na Mureith anaishi Uingereza na alikuwa amewafungulia biashara katikati mwa jiji la Nairobi na walikuwa wenye bidii sana.
Kamanda wa polisi kaunti ya Kajiado Muthuri Mwongera alisema uchunguzi umeanzishwa na waliohusika na mauaji hayo wanasakwa.
Mwongera alisema ingawa eneo hilo limekuwa na visa vingi vya wizi wa mifugo, wakazi hawangechukua sheria mikononi.
Aidha, familia imehamisha miili ya wapendwa wao kutoka katika City Mortuary na imepelekwa katika makafani ya chuo kikuu cha Kenyatta ambapo imehifadhiwa ikisuburi kuzikwa nyumbani kwao kaunti ya Nyandarua.
CHANZO - TUKO NEWS
Social Plugin