Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Watatu Waswekwa Rumande Kwa Ubadhirifu Wa Fedha Za Telesenta Sengerema


Na Faraja Mpina, SENGEREMA
Watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wanaosimamia Redio Sengerema 98.8 FM wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa ubadhirifu wa shilingi Milioni 27,720,000 ikiwa ni bakaa ya shilingi Milioni 103 zilizotolewa na taasisi ya mawasiliano ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ajili ya kuboresha Telesenta ya Sengerema

Maamuzi hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew baada ya kufika katika Telesenta hiyo na kusomewa taarifa ya matumizi ya fedha hizo iliyoonesha kuna bakaa ya shilingi Milioni 27,720,000 huku taarifa ya kibenki ya akaunti ya kituo hicho ikionesha fedha zote zimetumika na hakuna bakaa yeyote

Aidha, baada ya Mhandisi Kundo kuhoji kwanini taarifa ya kibenki inakinzana na taarifa waliyomsomea ndipo Meneja wa Kituo hicho Sostenes Tangalo kukiri kuwa wakati kituo kinapatiwa fedha na UCSAF suala la kurekebisha studio ya redio halikuwepo lakini katika manunuzi hayo ambayo yalifanyika kwa malipo ya fedha taslimu yaani cash wao wakaona wanunue na vifaa vya kurekebisha studio hiyo pamoja na samani

Baada ya maelezo hayo kuonesha kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha za Serikali zilizotolewa na taasisi ya UCSAF ambayo ipo chini ya Wizara hiyo Mhandisi Kundo ameagiza Meneja wa Kituo hicho Sostenes Tangalo, mwanasheria Ilambona Mahuba na Afisa Habari kuwekwa ndani na taratibu za kisheria zifuatwe bila kukiukwa ikiwa ni pamoja na watuhumiwa hao kupewa haki ya kusikilizwa pasipo manyanyaso ya aina yeyote

Sambamba na hilo ametoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya hiyo kuunda kamati maalum ya kuchunguza mchakato mzima wa manunuzi yaliyofanyika itakayowahusisha Ofisi ya TAKUKURU, Usalama, OCD na Wataalam wa TEHAMA na Manunuzi katika wilaya hiyo na taarifa sahihi kuwasilishwa Wizarani

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ameutaka uongozi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kupatiwa leseni ya kuendelea kurusha matangazo ya redio hiyo kwasababu leseni zinazotolewa huwa zina muda wa kutumika lakini pamoja na juhudi za TCRA kuwasiliana na uongozi wa redio Sengerema kwa ajili ya taratibu za kufuata zinazohusu leseni uongozi huo umekuwa ukikaa kimya

Mhandisi Kundo amezungumza hayo kujibu changamoto ya kusitishiwa leseni ya kurusha matangazo ya redio hiyo na TCRA iliyowasilishwa na Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com