Watu 24 wa familia moja wamefariki dunia baada ya kula chakula kinachoshukiwa kuwa na sumu kaskazini magharibi mwa Nigeria. Tukio hilo limetokea katika kijiji cha Danzanke - katika jimbo la Sokoto.
Kamishna wa Afya wa jimbo Ali Inname aliwaambia waandishi wa habari kwamba familia hiyo ilitumia kimakosa kemikali ya mbolea ambayo ilionekana kama chumvi wakati wa kuandaa chakula Jumatatu. Alisema wafanyikazi wa matibabu walijaribu kuokoa maisha ya wahanga bila mafanikio.
Hata hivyo watu wawili wa familia ambao walionja tu chakula hicho sasa wanapata matibabu hospitalini. Kufuatia tukio hilo, maafisa wameshauri tena watu kuweka vitu vyenye sumu mbali na maghala yao ya chakula kwa sababu za usalama.
Matukio kama hayo yanayohusu familia kufa kwa kula sumu yametokea huko Nigeria lakini idadi ya waliokufa katika tukio hili la hivi karibuni ni kubwa sana.