Waziri Mkuu Aitaka Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Kuangalia Upya Sheria Zake

 Waziri mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia upya sheria zake kuhusu katazo la kuvua samaki mchana katika ziwa Tanganyika

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Karema wilayani Tanganyika ambapo yupo mkoani katavi Kwa Ziara ya kikazi ya siku tatu

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo kufuatia maombi kutoka kwa mbunge wa jimbo la Mpanda vijijini Selemani Kakoso aliyemweleza Waziri Mkuu kuwa wavuvi wanakatazwa kuvua samaki mchana hali inayowafanya wavue usiku na kupata samaki wachache

Katika maombi yake Kakoso alisema japo Tanganyika wanakatazwa kuvua samaki mchana lakini mikoa ya jirani ya Rukwa na Kigoma wanaruhusiwa kuvua hali inayofanya wavuvi wa Katavi kuwa maskini

“Wenzetu wa Kongo wanavua mchana ziwa ni hili hili, halikadhalika Kigoma na Rukwa nao wameruhusiwa kuvua mchana. Sasa kwanini sisi hawa maafisa wetu wanatubania?” alihoji Kakoso

Hata hivyo Waziri Mkuu aliwapongeza wasimamizi wa ziwa wakiwemo Maafisa uvuvi kwa kusimamia sheria hiyo na kusema mikoa mingine inakosea

Mheshimiwa Waziri Mkuu pia amekagua ujenzi wa Bandari Mpya ya Karema na kuriddhishwa na maendeleo yake

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa bandari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania TPA mhandisi Erick Hamissi amesema ujenzi huo umefikia asilimia hamsini na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2022

Ameongeza kuwa awali bandari hiyo ilikuwa ianze kutumika mwezi Oktoba mwaka huu lakini kutokana na changamoto mbalimbali hasa za kuchelewa kufika kwa vifaa nchini kutokana na ugonjwa wa korona walilazimika kuongezewa muda mpaka Machi mwakani

Leo Waziri Mkuu atatembelea kiwanda cha kuchakata pamba kilichopo Ifukutwa na baadae atatembelea makazi ya Mishamo na kuzungumza na viongozi wa makazi hayo



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post