WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KUKWAMA KWA MITAMBO YA UJENZI WA KIWANDA CHA SUKARI CHA MBIGIRI


 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tixon Nzunda wakutane ili wakamilishe taratibu za utoaji wa mitambo ya ujenzi wa kiwanda cha Sukari cha Mbigiri.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Agosti 14, 2021) baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho, wakati alipotembelea mradi wa shamba la miwa la Mkulazi pamoja na kukagua ujenzi wa kiwanda cha sukari Mbigiri, mkoani Morogoro. Katika taarifa hiyo Waziri Mkuu alielezwa kuwa kuna baadhi ya mitambo ya ujenzi wa kiwanda imekwama bandarini.

“Tunataka kiwanda hiki kianze kujengwa, ucheleweshwaji usio na umuhimu hatuupi nafasi, hatutaki ujenzi ukwame, zile kontena 21 kule bandarini tunataka zitoke Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha na Mipango na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu mkae mkokotoe kile kinachopaswa kulipwa kijulikane mitambo ile itoke.

Waziri Mkuu amesema kwa namna nchi ilivyojipanga katika ujenzi wa viwanda, Tanzania itakuwa na viwanda saba vya sukari lengo likiwa ni kuhakikisha inajitosheleza kwa kuwa na sukari ya kutosha na kuondoa pengo la tani 70,000 lililopo, hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Mbali na maagizo hayo, Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Mkulazi, watendaji wa shamba la Miwa la Mkulazi pamoja na uongozi wa kiwanda cha Sukari cha Mbigiri kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kutokana na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa.

“…Kwetu sisi Watanzania mradi huu ni muhimu sana, nilikuja hapa mwaka 2018 sikukuta hali hii ninayoiona leo, miwa ilikuwa inaonekana kando kando ya barabara tu lakini leo nimekuta mabadiliko makubwa miwa inaonekana katika shamba lote na nimekuta harakati za ujenzi wa kiwanda cha sukari ambacho kipo katika hatua ya msingi, hongereni sana.”

Baada ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho cha Sukari cha Mbigiri, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wanaoishi pembezoni mwa eneo hilo walime miwa kwa wingi kwa kuwa wanasoko la uhakika la kuuza miwa. Pia ameuagiza uongozi wa wilaya ya Kilosa uhakikishe kila mwananchi anayetaka kulima miwa anapata ardhi kulingana na mahitaji yake.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha mazingira ya ukuaji wa uchumi nchini hususani kwa mwananchi mmoja mmoja, hivyo amewataka wananchi wachangamkie fursa za maendeleo zilizopo katika maeneo yao zikiwemo za kilimo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Medard Kalemani amempa siku saba Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Wilaya ya Kilosa awe amepelekea umeme katika visima vya wakulima wa miwa ambao kwa sasa wanatumia majenereta kuzalisha umeme.

Naye, Meneja wa shamba la Miwa la Mkulazi, Mhandisi Flavian Regonard amesema tayari wameanza kuvuna miwa katika shamba hilo na wanaiuza katika kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kwa kuwa bado hawajaanza uzalishaji wa sukari. “Eneo lililopandwa miwa kwa sasa ni hekta 2,705 na kwa mwaka huu wanatarajia kuendeleza shamba kwa kupanda hekta 800.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم