Waziri Nchemba Azindua Tume Ya Kutathmini Ukusanyaji Mapato Na Matumizi Ya Serikali


Na Rahma Taratibu, WFM, Dae es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mpiango Mh. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewapongeza wajumbe Tume ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali inayoongozwa na Profesa Samwel Wangwe walioteuliwa kwa kukubali uteuzi huo ili kushiriki katika kazi hii muhimu.

Ameyasema hayo wakati akizindua Tume hiyo jana katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es Salaam mahali ambapo hafla ya uzinduzi huo ilifanyika.

“Natambua kuwa mna majukumu mengi lakini kwa kutambua umuhimu wa suala hili na kutanguliza uzalendo mmekubali kuitikia uteuzi huu kwa ajili ya kutimiza jukumu muhimu na zito lililopo mbele yetu,”. Amesema Dkt.Mwigulu

Ameongeza kuwa kukamilika kwa kazi hii kutaboresha usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali na kuhakikisha tunakuwa na bajeti endelevu itakayoiwezesha Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Amesema Tume hiyo imejumuisha wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya Uchumi, Kodi, Fedha na Mifumo ya matumizi ya Serikali ambapo wajumbe hao wametoka taasisi mbalimbali za Tanzania bara na Zanzibar na wengine ni wastaafu katika nyanja hizo.

Aidha, amesema anatambua uwepo wa wajumbe wa Sekretarieti watakaofanya kazi sambamba na Tume hii ili kuhakikisha kazi hii inafanyika na kumalizika kwa wakati.

Kama tunavyofahamu nchi yetu imeendelea kuwa na kiwango kizuri cha ukuaji wa uchumi cha wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 kutoka mwaka 2011 hadi 2020.

Ameongeza kuwa ukuaji huu umeiwezesha nchi yetu kufikia hadhi ya uchumi wa pato la kati la chini mwaka 2020 ambapo  katika hali ya kawaida kiwango cha ukuaji wa uchumi wetu kinatarajiwa kiendane na ukuaji wa mapato ya ndani yanayoweza kutosheleza ugharamiaji wa matumizi ya Serikali ambayo nayo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

“Ni wazi kuwa uwezo wa nchi kukusanya mapato ni kigezo muhimu katika kuwezesha nchi kugharamia matumizi muhimu ya kiuchumi na kijamii kama vile elimu, afya, ujenzi wa miundombinu n.k.,” Amesema Dkt. Mwigulu Nchemba.

Wastani wa ukusanyaji wa kodi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 15.1 ya Pato la Taifa wakati kwa nchi zilizoendelea zinakusanya hadi asilimia 40 ya Pato la Taifa au zaidi.

Kiwango hicho kinaziwezesha nchi zilizoendelea kugharamia kikamilifu matumizi muhimu ya kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya kodi hapa nchini ni chini ya wastani wa ukusanyaji wa kodi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa mfano mwaka 2020/21, jumla ya mapato ya ndani yalikuwa asilimia 13.3 ya Pato la Taifa, ambapo mapato ya kodi yalichangia asilimia 11.2 ya Pato la Taifa.

Kiwango hiki kinadhihirisha kuwa Tanzania bado ina fursa ya kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi ili kufikia walau wastani wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wakati tukitafakari hali ilivyo kuhusu ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali, tukaona ni vyema kuwa na zoezi kubwa la kufanya tathmini ya mfumo mzima wa Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa kuunda Tume maalumu kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani ambao ni wabobezi katika masuala haya.

Amesema hili lingeweza kufanywa na Wizara ya Fedha na Mipango ama taasisi zake kama TRA, lakini kwa kutambua umuhimu wa kuwa na maoni huru na mawazo mbadala tumeona ni muhimu kuwa na tume hii.

Utaratibu wa kuunda Tume si mpya, bali umekuwa ukitumika katika kutatua changamoto za kitaifa kwa nchi nyingi duniani. Ipo mifano ya nchi zinazoendelea zilizoweza kufanya mageuzi katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato ambayo imeweza kuongeza mapato yake ya ndani.

Nchi hizo ni pamoja na Georgia, Guyana, Cambodia, Liberia na Ukraine. Mageuzi yaliyofanywa na nchi kama Georgia katika kipindi cha miaka ya 2004-2011 yaliwezesha nchi hiyo kukusanya zaidi ya asilimia 25 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 12 kabla ya mageuzi kufanyika.

Aidha, Nchi ya Guyana nayo ilianza kufanya mageuzi baada ya kupata mapendekezo ya Kamati ya kitaifa iliyojulikana kama National Tax Reform Committee (TRC) iliyofanya kazi mwaka 2016.

Vilevile, Mwaka 2018 Rais wa Afrika ya Kusini aliunda Tume iliyojulikana kama “Commission of Inquiry into Tax Administration and Governance by the South African Revenue Service” Tume hiyo iliundwa kufuatia kupungua kwa ukusanyaji wa mapato ya nchi hiyo.

Hivyo, kwa kutumia uzoefu wa nchi hiyo kuna nafasi kwa nchi yetu kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani.

“Napenda kuwakumbusha kuwa kazi kama hii iliwahi kufanyika mwaka 1991 ambapo Tume iliyoundwa kipindi hicho ilikuja na mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali zilizoonekana kuwa kero pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo yameleta matunda makubwa katika ukusanyaji wa mapato,”. Amesema Dkt Mwigulu.

Ndugu wajumbe, uzoefu kutoka nchi mbalimbali nilioueleza hapa unaonesha kuwa matokeo chanya katika ukusanyaji mapato yanaweza kupatikana kwa kufanya mapitio na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato.

Hivyo, ni muhimu kwa sasa Tanzania nayo ikafanya hivyo. Tathmini ya kina itasaidia kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia suluhisho ili kuboresha hali iliyopo ya makusanyo ya mapato ya Serikali.

Ni imani yangu kuwa Tume hii ninayoizindua leo itakuja na mapendekezo yatakayoboresha mfumo uliopo pamoja na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti endelevu.

Sehemu ya majukumu mahsusi ya Tume ni pamoja na:Kufanya tathmini ya mfumo wa kibajeti na kupendekeza namna bora ya kuiwezesha Serikali kuwa na bajeti endelevu;Kufanya ulinganishi wa Mfumo wa Kodi wa Tanzania na nchi nyingine zinazofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Kupitia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mifuko yenye vyanzo maalum na kushauri ipasavyo iwapo kuna haja ya kuendelea nayo au vinginevyo kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa bajeti ya Serikali;Kufanya tathmini ya mwenendo wa nakisi ya bajeti ya Serikali na kutoa mapendekezo kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya Serikali.

Jambo lingine ni kufanya tathmini ya ukuaji na ugharamiaji wa deni la Serikali, ulipaji wa mishahara, ulipaji wa malimbikizo ya madai/madeni na ukuaji wake; naKupitia gharama na taratibu za uanzishaji na uendeshaji wa biashara hapa nchini na kupendekeza namna ya kuboresha kodi zinazotozwa ili kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara hapa nchini.

Waziri Dkt. Mwigulu amemaliza hotuba yake kwa kuwashukuru tena wajumbe wa tume hiyo akithibitisha kuzindua rasmi Tume hiyo na nawatakia wajumbe utekelezaji mwema wa majukumu yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post