Waziri wa Kilimo Amtimua Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS)


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameagiza kuondolewa kwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) kilichopo katika Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) Bw. Nganga Nkonya na kuhamishiwa Wizarani kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.

Amesema kuwa kulikuwa na uhujumu wa kiutendaji katika mfumo BPS ikiwa ni pamoja na msimamizi huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa mujibu wa matakwa ya serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya kutosha na kwa wakati

Waziri Mkenda ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wafanyabiashara wa mbolea uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.

“Sisi mbolea ni suala la kufa na kupona sio suala la mzama kama alivyokuwa anafanya, kulikuwa na mtu anajaribu kucheza na mfumo huo jambo lililopelekea kuchelewa kwa upatikanaji wa mbolea kwa wingi na kwa wakati” Amekaririwa Mhe Mkenda

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kufanya mapitio ya mfumo huo ambapo itaendelea kutafuta namna nzuri ya kumsaidia mkulima kwa ajili ya upatikanaji wa mbolea.

Kuhusu bei ya mbolea kupanda, Waziri Mkenda amesema kuwa hilo ni tatizo la Dunia nzima kwani soko la Dunia limepanda kwa kiasi kikubwa ikiwemo gharama za usafirishaji.

Ameeleza kuwa pia tayari Serikali imeielekeza Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo.

Ili kuongeza ufanisi zaidi wa utendaji Waziri Mkenda amesema kuwa vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم