SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MIFUMO YA UPATIKANAJI WA DAWA NA VIFAA TIBA


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kujidhatiti vyema katika upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kutolea huduma kama sehemu ya maandalizi kuelekea utekelezaji sheria ya bima ya afya kwa wote.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akikagua vifaa vya vipimo vya maabara vilinunuliwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala kutoka MSD kwa bei nafuu zaidi chini ya asilimia 50 ukilinganisha na bei ya awali. 

"Jana nilikuwa MSD kufanya ufuatiliaji wa hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa vya maabara kwa gharama nafuu kupitia maboresho ya MSD na leo nimekuja hapa Mwananyamala kuangalia iwapo kweli vifaa vya maabara kwa gharama nafuu vimefika? nimeona zipo hatua MSD inafanya na taasisi zingine pia zinafanya ili kupunguza gharama za huduma",amesema

Amesema kuwa, MSD imepitishiwa Sheria yake ya kutengeneza dawa, na tayari dawa zinazalishwa Keko na hivi karibuni uzalishaji utaanza kwenye viwanda vya Makambako vilevile,  tayari watu binafsi wamekuja kuwekeza katika uzalishaji wa dawa nchini, hali itayosaidia kuondokana na changamoto ya upungufu wa dawa nchini na pia kupata nafuu ya bei na uharaka wa kupata bidhaa hizo.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa, sehemu kubwa ya maandalizi ya safari ya kuelekea kwenye sheria ya bima ya afya kwa wote imekalika na ifikapo Novemba Serikali itapeleka mswada wa Sheria ya Bima ya Afya ili ujadiliwe Bungeni na kila mwananchi awe na Bima yake ya Afya ambayo itamwezesha kupata huduma, huku akibainisha kwa watu ambao hawana uwezo kabisa watabainiwa kwa utaratibu uliopo nchini na kuina namna watavyosaidiwa. 

"Tumekuwa tukisema kwamba tupo kwenye maandalizi ya kupeleka mswada wa Sheria ya Bima ya Afya ukajadiliwe bungeni ili kila mwananchi awe na Bima yake ya Afya ambayo itamwezesha kupata huduma na kwa wale watu ambao hawana uwezo kabisa watabainiwa kwa utaratibu uliopo nchini " ,amesema Dkt. Gwajima. 

Aidha, Dkt. Gwajima amedai kuwa, tayari bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetenga karibu Bilioni 149 ili kuainisha wananchi wote ambao hawana uwezo ili kupatiwa nafasi ya kuwa na Bima itakayowasaidia kupata huduma za Afya baada ya kuanza kwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote. 

Mbali na hayo, Dkt. Gwajima amesema kuwa mashine hizo za Maabara zilizofungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala zitaendelea kusambazwa maeneo yote nchini ili kusogeza huduma bora kwa wananchi kwa bei nafuu, huku akisisitiza kuwa ifikapo mwisho wa Disemba mwaka 2021 vituo vyote vitakuwa vimefungwa nchini.

Kama Serikali, tumekubaliana ifikapo Januari mwaka 2022 vituo vyote nchini vitakuwa vina mashine hizo sambamba na upatikanaji wa huduma za vipimo husika kwa bei nafuu zaidi amesema Mhe. Waziri wa Afya Dkt. Gwajima. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post