Picha haihusiani na habari hapa chini
Kijana aliyejulikana kwa jina la Michael Jackson (25) mkazi wa Kijiji cha Magara wilayani Babati mkoani Manyara ameuawa kwa kukatwa katwa mapanga baada ya kumfumania akichovya asali (akifanya mapenzi) kwenye banda la ng’ombe na mke wa Samwel Alfred (48) aitwaye Habiba Saidi (22).
Semasema kijijini hapo zinaeleza kuwa Michael Jackson ambaye bado ni kijana alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke huyo wa mtu kwa muda mrefu na alionywa mara nyingi na siku ya tukio jamaa mwenye mke 'Alfred' ambaye alikuwa amepewa taarifa kuhusu tabia ya kijana huyo kuhondomola mke wake aliweka mtego ili aweze kuwafumania.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), Merrison Mwakyoma tukio hilo limetokea majira ya saa 10 alfajiri ya Septemba 8,2021.
"Siku ya tukio Alfred alimuaga mkewe Habiba majira ya saa 10 alfajiri kuwa anakwenda kukata kuni na kumuacha mkewe akiwa amelala lakini mkewe huyo akampigia simu hawara yake aitwaye Michael Jackson aende nyumbani kwake wakafanye mapenzi kwani mme wake hayupo",amesema.
"Hawara yake huyo Jackson baada ya kufika nyumbani kwa Alfred baada ya kupigiwa simu na Habiba kisha walizunguka kwenye banda la ng’ombe na kutandika mgorore chini na kuanza kuvunja amri ya sita lakini ghafla mumewe alirudi na kuwafumania wakifanya mapenzi ndipo Alfred akiwa na panga mkononi alilitumia kumkata sehemu mbalimbali za mwili mpaka akafariki dunia na mkewe ambaye alikuwa anamzuia asiendelee kumjeruhi marehemu naye alikatwa mkono ukadondoka chini",ameeleza Kamanda Mwakyoma.
Tayari Jeshi la Polisi Mkoani Manyara linamshikilia Samwel Alfred (48), mkazi wa Kijiji cha Magara wilayani Babati kwa tuhuma za kumuua Michael Jackson (25) na linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na litamfikisha mahakamani mtuhumiwa baada ya uchunguzi kukamilika.
"Natoa wito kwa jamii kuwa waoga katika kutembea na wake za watu kwani wivu wa mapenzi ni matukio yanayojitokeza mara kwa mara. Wananchi wanatakiwa kuacha mapenzi yasiyo na tija kila mmoja achukue tahadhari", amesema Kamanda Mwakyoma.