MCHEZAJI Sunday Justine ambaye alikuwa klabu ya Pamba Football Club msimu uliopita amesajiliwa na Gwambina Football Clu ya Misungwi Mkoani Mwanza kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Sunday ambaye hucheza beki ya kulia, amedumu katika timu ya Pamba kwa Miaka Miwili wakipambania Kuipandisha Ligi Kuu ingawa bahati haikuwa hivyo. Kabla ya kwenda Pamba alitokea Kamunyange FC ya Mkoani Kagera.
Akizungumzia usajili wake kwenye timu ya Gwambina, Sunday amesema amefurahi kupata nafasi hiyo adhimu ambayo itampa nafasi ya kuonyesha kipaji chake ambacho Mungu amempa, kwa ushirikiano na wachezaji wenzake waweze kuirudisha Gwambina Ligi Kuu Msimu ujao.
Sunday ambaye yuko chini ya Famara Sports Management amesema anajisikia fahari kupata nafasi hiyo kwenye timu yake mpya ya Gwambina FC na kuushukuru uongozi wa timu ya Pamba kwa kumuamini kwa muda wote aliokaa klabuni hapo.
"Nina furaha sana, kwanza kupata nafasi hii, maana Kazi ya Mchezaji yoyote ni kucheza mpira. Nimepata nafasi Gwambina acha nikafanye kazi, pia niwashukuru Pamba kwa kuniamini kwa muda niliokaaa nao",alisema Sunday Justine.
Sunday ni mmoja wa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu ya Gwambina Football Club ambayo Msimu uliopita ilikuwa Ligi Kuu na Msimu huu ikitarajia kucheza Championship (Ligi Daraja la Kwanza) Tanzania Bara.
Social Plugin