Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akifungua mafunzo ya siku nane kwa wanafunzi 50 wa taasisi za elimu ya juu wanataaluma wa TEHAMA yanayotolewa na Kampuni ya HUAWEI Tanzania kupitia program yao ya Seeds for the future jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) akiwemo Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Albina Tenge (Kulia), Naibu Mkurugenzi Mkuu wa HUAWEI Tanzania Bw Tom Tao (wa pili kushoto – walioketi) pamoja na wanafunzi wanufaika wa Mpango wa kuibua vipaji vya TEHAMA kupitia mafunzo vyuoni, ulioasisiwa na kampuni ya Huawei unaofahamika kama ‘Seeds for the Future Program’. Hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jiji Dodoma.
Na Mwandishi, wetu
Serikali imeahidi kushirikiana na kuunga mkono jitihada za kampuni ya Mawasiliano ya Huawei katika kuweka mkazo zaidi na kuwaendeleza wanawake katika sekta ya TEHAMA ili kuongeza uwiano wa kijinsia baina ya wanawake na wanaume katika sekta hiyo.
Ahadi hiyo ya serikali ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainabu Chaula wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango wa kuibua vipaji vya TEHAMA kwa vijana kupitia mafunzo vyuoni, ulioasisiwa na kampuni ya Huawei unaofahamika kama ‘Seeds for the Future Program’ iliyofanyika mwishoni mwa wiki jiji Dodoma.
Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta TEHAMA, imejipanga kushirikiana na kampuni hiyo kuhakikisha inautumia vema mpango huo na mipango mingine kama hiyo kuzalisha vijana wenye weledi wa kutosha kuhusu masuala ya TEHAMA huku suala la usawa wa kijinsia pia likipewa kipaumbele.
“Tunaamini kupitia ushirikiano huu tunaoupata kutoka kwa wenzetu kampuni ya Huawei tutafanikiwa kukamilisha adhima hii. Pamoja na kuipongeza kampuni ya Huawei kwa kwa kutekeleza mpango huu kwa mwaka wa sita sasa naendelea kuwahakikishia ushirikiano mzuri zaidi kutoka serikalini ili kwa pamoja tufikie malengo,’’ alisisitiza.
Aidha, Dkt. Chaula alisema kuwa fursa nyingi zinapatikana kupitia TEHAMA na kati ya vijana 50 watakaopatiwa mafunzo hayo vijana 40 ni wasichana kitu ambacho kinatia moyo na kutoa hamasa kwa vijana hasa kutokana na ushuhuda wa moja ya wanufaika wa programu hiyo Bi. Emilina Masanja kutoka chuo kikuu cha Mzumbe aliyesema kupitia TEHAMA amekuza biashara yake kwa kuongeza wigo wa wateja ambao wengine wapo nje ya nchi
Katika hatua nyingine Dk Chaula alitoa wito kwa vijana nchini kutumia vema maendeleo ya TEHAMA kwa kubuni fursa mbalimbali zinazoweza kutokana na sekta hiyo kwa maendeleo yao binafsi na maslahi mapana ya nchi ikiwemo mafunzo na fursa za ajira badala kutumia ukuaji wa sekta hiyo kufanya vitendo vilivyo kinyume na maadili ya jamii na taifa kwa ujumla ikiwemo utapeli na makosa mengine kupitia mtandao.
Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa HUAWEI Tanzania Bw Tom Tao alisema kuwa mafunzo hayo yameanza kutolewa mwaka 2016 kwa kuchagua wanafunzi 10 wa TEHAMA wanaofanya vizuri kutoka katika taasisi za elimu ya juu kwa kuwapatia mafunzo ya teknolojia za kisasa katika TEHAMA nchini China na pia kujifunza utamaduni wao
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto za UVIKO 19, kuanzia mwaka jana mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa njia ya mtandao na idadi ya wanafunzi hao kuongezeka kutoka 10 hadi kufikia wanafunzi 50 ambapo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 150 wamenufaika na programu hiyo
Alisema katika kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inafanikisha mkakati wake wa kuongeza usawa wa kijinsia kwenye sekta ya TEHAMA, asilimia 90 ya wanufaika wa mpango huo kwa mwaka huu ni wanawake.
“Zaidi, Huawei inatambua umuhimu wa elimu ya TEHAMA katika uletaji wa maendeleo ya nchi, hivyo imejidhatiti kuhakikisha kuwa kupitia program hii na program nyingine za Huawei vijana wanapata elimu sahihi ya TEHAMA katika teknolojia za kisasa kabisa ili kupanua ujuzi na maarifa yao na kuwafanya wawe na sifa za ushindani katika soko la ajira.’’ Alisema
Akizungumza kwenye hafla hiyo, mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM) Prof. Albina Tenge alisema kuwa chuo hicho kina ndaki ambayo inafundisha taaluma ya teknolojia ya habari na mawasiliano inayoitwa CIVE, hivyo programu ya HUAWEI Tanzania ya Seeds for the Future inatoa hamasa kwa vijana wanaochukua kozi za TEHAMA kwa kuwapa nafasi ya mafunzo kwa vitendo na pia inawezesha vijana hao kuweza kujiajiri na kuajirika
Awali, wakielezea hisia zao kuhusu mpango huo, baadhi ya wanafunzi wanufaika wa mpango huo, Bi Eveline kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Mmorogoro pamoja Henry Materu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na kuishukuru kampuni ya Huawei kwa mpango huo, walisema watahakikisha wanatumia vema mafunzo hayo ya TEHAMA kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii ikiwemo kufanya vumbuzi zitakazochochea maendeleo ya kijamii ikiwemo kuongeza ajira kwa vijana.
Social Plugin