Kumeshuhudiwa kizazaa kwenye hafla moja ya mazishi kaunti ya Kakamega nchini Kenya baada ya mwanaume mmoja kunaswa akimwekea marehemu mayai kwenye jeneza huku ibada ikiendelea.
Imeripotiwa kuwa Benson Mumia 60, mkaaji wa eneo bunge la Lurambi, alifika kwenye hafla hiyo katika kijiji cha Eshiakhulo, eneo bunge la Mumias mashariki na kufululiza hadi kwenye jeneza la marehemu alikofumaniwa akitekeleza mazingaumbwe hayo.
Kulingana na Jane Aseka ambaye ni mkwe wa marehemu, alimfumania mshukiwa akiweka mayai mawili karibu na kichwa cha marehemu alipokuwa ameenda kuukagua mwili kabla ya kufunika jeneza na kumwandaa kwa mazishi.
’Nikamuona na mayai mawili. Akaweka moja upande wa kushoto na lingine upande wa kulia wa kichwa cha mwendazake,’’ alisema
Aseka kabla ya kupaza sauti kuwajuza waombolezaji alichokiona.
Ni kisa kilichowaghadhabisha waombolezaji ambao walimgeukia mshukiwa na kumpokeza kichapo cha mbwa huku ibada ikisitishwa kwa muda.
"Tangu nizaliwe sijawai ona kisa kama hiki, atueleze anahusika kivipi na kifo cha marehemu ikizingatiwa kifo cha marehemu ni cha kushtukaniwa," Akasema Stela Musimbi mmoja wa waombolezaji.
"Huu ni ushirikina mtupu, huenda alihusika kwa kifo cha mama,’’ Sauti nyingine kutoka kwa umati ikasikika.
Aidha, ilimbidi askofu Simon Malenya wa kanisa la Faith Beleivers aliyekuwa akiendesha ibada kuingililia kati na kumuokoa mshukiwa huyo kutoka kwa mikono ya waombolezaji.
Hata hivyo, kulingana na wazee wa jamii hiyo wakiongozwa na Josphert Shitsama, walisema huenda mshukiwa alihusika na kifo cha mwendazake na kwa yeye kuweka mayai hayo ilikuwa ni njia ya kuzuia mazimwi kutoka kwa marehemu yasimuandame.
"Alimwekea mayai ili alale kabisa asiwai amka kumsumbua tena," Akasema Shitsama.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin