Na Adelinus Banenwa - Bunda
Kijana aitwaye Jumanne Jackson (21) mkazi wa mtaa wa Kabusule Kata ya Nyamakokoto Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu tumboni na kifuani na kijana mwenzake Chacha Mangeo (21) katika ugomvi wa fedha shilingi 1000 ya kamali.
Mashuhuda wamesema tukio hilo limetokea Septemba 28, 2021 jioni ambapo wameeleza kuwa walisikia ugomvi katika chumba alichokuwa akiishi Marehemu Jumanne Jackson (21) na baada ya kutoka nje walimuona mtuhumiwa Chacha Mangeo akikimbia huku Jumanne akiwa ameinama huku damu zikichuruzika chini kutoka tumboni na kifuani.
Mmoja ya ndugu wa marehemu huyo alisema “Nilisikia mlango unagonga puuuuh sikushtuka maana hii milango inatumia nguvu kuifungua, Ila kabla sijakaa vizuri nikaitwa... bibi bibi wanagombana huku, nilipotoka nje nikakuta wanasukumana huyu kijana aliyefariki na kijana aliyekuwa anagombana naye (Chacha Mangeo) akiwa ameshika kisu kikiwa na damu, walitoka nje Jumanne aliinama chini huku damu zikiwa zinamtoka ghafla akachomwa kisu kingine kisha mtuhumiwa akakimbia”.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara Longinus Tibishubwamu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akisema chanzo ni ugomvi wa kamali ambapo marehemu Jumanne Jackson alishinda sh. 1000 jambo ambalo mtuhumiwa hakukubaliana nalo na kuamua kumshambulia kwa kisu na kusababisha kifo chake.
Aidha kamanda Tibishubwamu amesema mtuhumiwa anashikiliwa kituo Cha Polisi Bunda na mwili wa Marehemu umehifadhiwa Hospitali ya DDH Bunda.
Kamanda Tibishubwamu ametoa wito kwa jamii kuvumiliana na kuwa na utu ili kuacha matendo mabaya.
Social Plugin