Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Watu watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya gari lenye namba za usajili T.111 CUU aina ya Mitsubish Fuso lililokuwa kugongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T.612 BNN aina ya Mitsubish Canter katika eneo la Konoike kijiji cha Kolila wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo Septemba 08, 2021 majira ya saa 10:00 alfajiri huko Barabara ya Arusha/Moshi eneo la Konoike kijiji cha Kolila Tarafa ya King’ori wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha ambapo kulitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu watano na majeruhi mmoja.
Kamanda Masejo amesema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ambapo gari lenye namba za usajili T.111 CUU aina ya Mitsubish Fuso lililokuwa linaendeshwa na Heriel Jinja Lyimo (42) Mkazi wa Holili mkoani Kilimanjaro liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T.612 BNN aina ya Mitsubish Canter iliyokuwa ikiendeshwa na Peter Mmasi ambaye bado umri wake na makazi yake hayajafahamika.
ACP Masejo amesema uchunguzi wa awali umebaini kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha ambapo ilihama upande wa pili wa Barabara na kugongana na gari aina ya Mitsubish Canter lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Moshi.
Aidha baada ya magari hayo kugongana gari aina Mitsubish Fuso lilipitiliza na kuanguka kwenye mtaro uliopo pembezoni mwa barabara.
Kamanda Masejo amesema kuwa waliofariki katika ajali hiyo ni Peter Mmasi ambaye ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter, Victor Kileo , Vivian Urio na Isack Temba ambao walikuwa abiria wa gari aina Mitsubishi Canter na ni wakazi wa Baraa jijini Arusha na katika gari aina ya Mitsubish Fuso aliyefariki ni utingo wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Idd mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro.
Katika taarifa yake amesema kuwa Majeruhi katika ajali hiyo ni Heriel Jinja Lyimo ambaye amepelekwa katika hospitali ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Jijini Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini na matumizi sahihi ya alama za usalama Barabarani ili kuepusha madhara makubwa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai na uharibifu wa vyombo vya moto wanavyotumia