RAIS SAMIA AIDHINISHA BILIONI 207 KURAHISISHA UPATIKANAJI MAJI VIJIJINI


Waziri wa Maji Jumaa Aweso
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph 

Na Dotto Kwilasa -  Dodoma
WAZIRI wa Maji nchini Jumaa Aweso amesema Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kiasi cha shilingi Bilioni 207 kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa maji Vijijini ikiwa ni dhamira yake ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Aweso ameyasema hayo Jijini Dodoma kwenye mkutano wake na vyombo vya Habari nchini uliolenga kutoa shukrani kwa vyombo hivyo kwa namna ya pekee ambavyo vimetoa ushirikiano kwenye Wizara hiyo na kupelekea kupatikana kwa mafanikio mbalimbali.

Amefafanua kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya maji nchini kwa nia njema Rais Samia katika Bunge la Bajeti ameidhinisha Bilioni 680 kwa Wizara hiyo ili kwenda  kutekeleza miradi ya maji mijini na  vijijini na kutatua kero ya maji.

Hatua hii imekuja huku Wizara hiyo ikiwa katika mkakati wa kuhakikisha  inafikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini huku ikipata fedha Zaidi ya dola milioni 500 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi Tirion moja  iliyotokana na mahusisano mazuri kati ya Tanzania na Serikali ya India kupitia Exim Bank.

Waziri huyo wa Maji ameeleza kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi ya Maji katika miji 28 na kwamba vibali tayari vimepatikana na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni hali itakayosaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

“Mojawapo ya Miji hiyo ni                            Makambako,Wanying’ombe,Muheza,Handeni na maeneo mengine ili kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji ya watanzania mijini na vijijini”, amesema.

Licha ya hayo ameeleza kuwa katika maeneo ya Vijijini kupitia fedha zilizoidhinishwa na Bunge pamoja na zilizoongezwa na Rais Samia ,Wizara kwa kushirikiana na wakala wa maji vijijini (RUWASA)itaendelea kutoa maelekezo mahsusi kwa wahandisi wote wa maji kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata maelekeo ya wizara hiyo ili kutatua kero ya maji.

Pamoja na mambo mengine, ameeleza kuwa ili kuhakikisha Wizara hiyo inafanikiwa kuingia asilimi 85 ya upatikanaji wa maji Vijijini ,kwa mwaka huu imepanga kuingia mikataba 1176 kwa ajili ya kuhakikisha wanajenga miradi ya maji vijijini kwa kuzingatia kuwatumia wakandarasi wenye uwezo.

“Tumezingatia Wakandarasi wasio na uwezo hawatapata miradi,wakandarasi wazuri wanafahamika na wakwamishaji wanafahamika,moja ya changamoto ya ukwamishaji wa miradi ya maji ni wakandarasi wababaishaji wasio na uwezo hatuwezi kuwapa nafasi kwenye wizara yetu,”ameeleza.

Pia Aweso amewataka Wakandarasi watakaoingia mkataba na wizara hiyo kulichukulia suala la maji kama vita mahsusi ya kuhakikisha watanzania waishio vijijini wanaondokana na kero ya maji na kuwa na uhakika wa kupata maji wakati wote.

“Si busara hata kidogo kuona leo mradi wa maji unakwamishwa kwa kukosa fedha kwa ajili ya ubadhilifu,tunataka wananchi wapate manufaa kutokana na serikali yao hakuna usiri wowote kwenye miradi hii ya maji,tunataka kila kitu kiwe wazi,”amesema.

Katika hatua nyingine ,Waziri huyo mwenye dhamana ya usimamizi wa maji nchini amezungumzia hali ya upatikanaji wa Maji kwa Jiji la Dodoma ambapo ameeleza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa maji ambapo uwezo wa uzalishaji wa maji kwa sasa ni lita milioni 66 huku mahitaji yakiwa ni lita 103 kutokana na ongezeko la watu.

Kutokana na hayo,Aweso ameeleza kuwa zipo jitihada ambazo wizara hiyo imefanya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma(DUWASA) kwa kuchimba visima maeneo ya pembezoni na kuongeza tenki kubwa eneo la Buigiri  ili kuhakikisha maeneo ya Soko la Ndugai,Nzuguni,Njedengwa yanapata maji ifikapo mwezi wa kumi mwaka huu.

Akieleza kuhusu azma ya mkutano wake na Waandishi wa Habari,Waziri Aweso ameeleza kuwa bila vyombo vya Habari wizara yake isingefanikiwa .

Amefafanua kuwa kupitia vyombo vya Habari wananchi wamekuwa wakipa taarifa mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa maji na kuwafanya kuendele kuzitatua changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amewatoa wasiwasi wakazi wa Jiji la Dodoma kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya maji itahakikisha inatatua kero zote za maji kwa kufanikisha miradi yote ambayo inaendelea kutekelezwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post