Mfanyabiashara wa Rwanda amepigwa risasi na kuuawa katika manispaa ya Matola, kilomita chache kutoka mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.
Levocat Karemangingo alipigwa risasi takribani mita 50 kutoka kwenye makazi yake yaliyopo katika makazi ya Liberdade, Jumatatu asubuhi.
Imedaiwa kuwa uhalifu huo ulifanywa na majambazi waliokuwa katika magari matatu ambao walilizuia gari lake kabla ya kummiminia risasi.
Wauaji hao hadi sasa hawajajulikana, jambo lililoitikisa jamii ya Wanyarwanda wanaoishi Msumbiji.
Polisi walikuwa kwenye eneo la tukio kufanya uchunguzi wa mwili wake na mwili wake ulipelekwa kwenye hospitali ya jimbo.
Baadhi ya Wanyarwanda wamewaambia waandishi wa habari kuwa uhalifu huo uliwalenga raia wanaopinga serikali ya sasa ya Rwanda na kudai kuwa watu wengi wanalengwa.
Wanyarwanda walioko Msumbiji wameiomba serikali kuwapatia ulinzi zaidi. Mwaka 2019, Mnyarwanda mwingine, Louis Baziga, aliuawa kwa risasi katika kitongoji cha Maputo baada ya watu wenye gari kuzuia gari lao. Alifahamika kuunga mkono serikali ya Rwanda.
Social Plugin