Serikali ya Sudan inasema kumekuwa na jaribio la mapinduzi lililotibuka katika nchi hiyo na hatua zinachukuliwa kudhibiti hali hiyo, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.
"Kumekuwa na jaribio la mapinduzi lililoshindwa, watu wanapaswa kukabiliana nalo, "Shirika la habari la AFP linanukuu ripoti zikisema.
Kulikuwa na jaribio la kuchukua jengo ambalo lina vyombo vya habari vya serikali, Shirika la habari la AFP linasema likiashiria chanzo cha serikali.
Msemaji wa serikali amesema shughuli ya kuwahoji wanaoshukiwa kuwa nyuma ya jaribio hilo la mapinduzi itaanza muda mfupi ujao.
Msemaji huyo aliyenukuliwa na mashirika ya habari ya kimataifa anasema wapangaji wa mapinduzi walijaribu kuchukua udhibiti wa redio ya Serikali huko Omdurman, ng'ambo ya mto Nile kutoka mji mkuu Khartoum.
Maandamano yalikuwa yamepangwa kufanyika mjini Khartoum leo na wanajeshi walikuwa wametumwa kushika doria mitaani wakati mapinduzi hayo yalipojaribiwa.
Serikali ya mpito ya Sudan ambayo imekuwepo tangu 2019 imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kuleta mageuzi ya kiuchumi na kisiasa licha ya madai yanayokinzana kutoka kwa maeneo ya kihafidhina na yale huria.
Chanzo - BBC Swahili