Wafanyakazi wa kiwanda cha Nondo waliolipukiwa na uji wa moto
Wafanyakazi 40 wa kiwanda cha Nondo cha Nyakato jijini Mwanza, wamejeruhiwa na mlipuko wa moto uliotokea kiwandani hapo jana Septemba 24, 2021, baada ya kinu cha uji wa moto kulipuka ambapo waliokuwa karibu ndiyo walioathiriwa zaidi na joto la uji wa vyuma.
Majeruhi hao walifikishwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, na kupokelewa na daktari wa magonjwa ya jumla wa hospitali hiyo Dkt. Diana Anatory, ambapo amesema baadhi yao walikuwa wanalalamika kuwa na shida ya upumuaji pamoja na kuwa na majeraha ya mwilini.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mwanza, Ambwene Mwakibete, alisema mlipuko huo wa joto la uji wa vyuma umewaathiri wafanyakazi waliokuwa eneo hilo na wengine waliokua mbali wameathirika kwa kurukiwa na uji huo na amewataka wamiliki wote wa viwanda kuchukua tahadhari kwa wafanyakazi wao kwa kuhakikisha wanavaa vifaa vya usalama na kujikinga na madhara ya moto.
Aidha kwa mujibu wa taarifa ya daktari majeruhi 33 waliruhusiwa kurudi nyumbani na majeruhi saba walilazwa.
Chanzo - EATV