Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEC YAANIKA KATA, MAJIMBO YA UCHAGUZI MDOGO..YAWATAKA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI KUACHA MAZOEA


Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mst) Mary Longway, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata yanayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia leo 10 hadi 12 Septemba,2021.

Na Mwandishi Maalum, Morogoro

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Ushetu katika Halmashauri ya Ushetu Mkoani Shinyanga na Kata za Tanzania bara kutokufanya kazi ya Uchaguzi kwa mazoea na badala yake wazingatie maelekezo, kanuni na sharia za uchaguzi katika utendaji wao.

Tume pia imewataka wasimamizi hao na wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanavishirikisha Vyama vyote vya Siasa na Wadau wengine ili kurahisha utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (Mst) Mary Longway wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata yanayofanyika Mkoani Morogoro.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, ni vyema mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea”,alisema Jaji (Mst) Longway.

Aidha amewataka kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na kwamba katika utendaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume na kuongeza kua jambo hilo lisiishie katika mafunzo na nadharia bali ionekane kufuatiwa katika kutenda.

“Sanjari na hilo nawaasa kukumbuka kuvishirikisha Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia sana utekelezaji wa majukumu yenu,”alisema Jaji (Mst) Longway.

Wasimamizi hao wametakiwa kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vizuri maeneo ambayo chaguzi utaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika Kata na hasa Vituo vya kupigia kura.

“Mfanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani,”alisema Jaji (Mst) Longway.

Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mst) Mary Longway pia amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana kuacha na undugu au upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

Jaji (Mst) Lougway, alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri ,wenye ufanisi na hivyo utasaidia kuondoa malalamiko au vurugu wakati wa uchaguzi.

Alisema jambo muhimu wanalotakiwa kuzingatia Wasimamizi hao wa uchaguzi ni kujiamini na kufanya kazi kwa weredi na kuzingatia Katiba ya nchi,sheria za uchaguzi na kanuni zake,maadili ya uchaguzi pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume.

Aidha Mjumbe wa Tume hiyo ya uchaguzi,aliwasisitizia wasimamizi hao wa uchaguzi kuhakikisha wanafanya utambuzi wa vituo vya uchaguzi mapema kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Hata hivyo Jaji huyo Mstaafu alionya wasimamizi hao wa uchaguzi kuachana na udugu na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi na badala yake wawajiri watendaji wa vituo wenye weredi na wanaojitambua kadri inavyowezekana.

Hata hivyo Mjumbe wa NEC aliwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya,Jinsia na Watoto juu ya kujikinga na UVIKO 19 wakati wa kipindi chote cha uchaguzi.

“Kama mnavyotambua tupo katika wimbi la maambukizi ya UVIKO 19, kwa kuzingatia kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya , Jinsia, Wazee na Watoto juu ya kujikinga na maambukikizi dhidi ya ugonjwa huu, Tume inaendelea kuwaasa na kusisitiza kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu wa Afya kwa kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha ikiwemo; Kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni, Kutumia Vitakasa mikono (Sanitazer) na Kuvaa Barakoa,” alisema Jaji (Mst) Longway.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Uchaguzi,Emanuel Kawishe,akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume, alisema uchaguzi huo mdogo utafanyika katika Jimbo la Konde (Zanzibar) na Jimbo la Ushetu (Shinyanga) pamoja na kata 10 za udiwani.

Alizitaja Kata hizo na Halmashauri zake katika mabano ni Kileo (Mwanga DC), Neruma(Bunda)Kagera–Nkanda(Kasulu DC) Luduga(Wanging’ombe), Vumilia (Urambo),Lyowa (Kalambo),Buyuni(Ilala), Dongo(Kiteto, )Lighwa(Ikungi) na Ndembezi (Shinyanga).

Mapema kabla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo wasimamizi hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujiondoa uanachama wa vyama vyao vya siasa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Maua Rashid Hamduni

Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mst) Mary Longway, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata yanayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia leo 10 hadi 12 Septemba,2021.



Baadhi ya washiriki ambao ni wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata wakifuatilia mafunzo ya usamizi wa uchaguzi yaliyoanza leo Septemba 10 na kumalizika Septemba 12,2021 mkoani Morogoro.


Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Uchaguzi,Emanuel Kawishe,akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume.




Hakim Kazi Mfawidhi Maua Rashid Hamduni akizungumza wakati wa kuwaapisha Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wa Saidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata wakati wa kuanza mafunzo yao mkoani Morogoro.




Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wakila kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi ,Maua Rashid Hamduni ambapo walikula kiapo cha kutunza siri na kujiondoa kuwa wanachama wa vyama vya siasa.


Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wakisaini hati za kiapo baada ya kula viapo vya kutunza siri na kujiondoa kuwa wanachama wa vyama vya siasa.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com