Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO AWATAKA WATANZANIA KUTUNZA MAZINGIRA KULINDA ANGA LA HEWA 'OZONE LAYER'

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo

 Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Ikiwa  ni maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuhifadhi tabaka la Ozoni, Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo ametumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa umma na kuwataka watanzania  kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kununua bidhaa rafiki wa Ozoni (Ozone friendly) ili kulinda tabaka hilo dhidi ya uharibifu.

Waziri huyo mwenye dhamana ya mazingira nchini amebainisha hayo jijini hapa alipofanya ziara kwenye maduka ya viafaa vya umeme pamoja  na mafundi wanaojishughulisha na uuzaji na utengenezaji wa majokofu na viyoyozi katika maadhimisho yakupambana na kulilinda anga la hewa (Ozone layer).

Amesema,Ozoni  ni tabaka la hewa ambalo liko katika anga la juu la pili lifahamikalo kitaalamu kama stratosphere ambalo linaweka aina ya tabaka ama tambara angani ambalo linazuia mionzi mikali ya jua inayoweza kuleta athari katika afya za binadamu na viumbe hai kuja moja kwa moja duniani.

Mbali na hayo ameeleza kuwa uharibifu wa tabaka la Ozoni unapelekea madhara mbalimbali duniani ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani pamoja na kuleta mabadiliko ya tabia ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu na viumbe hai.

"Wanyabiashara acheni  kuuza Majokofu na Viyoyozi vya mtumba kwani vimeonekana kuleta athari kubwa katika vizazi vyetu vya sasa na vijavyo,wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuza majokofu ya mtumba yalikuwa yakitumia gesi R22 ambayo yalikuwa ikiharibu mazingira ambapo bidhaa hizo zinazoletwa kutoka katika nchi za nje zimekuwa zikileta madhara makubwa katika Anga la hewa , uzeni mitungi ya gesi kuanzia R200 na kuendelea,"ameeleza.  

Jaffo ametoa wito kwa vijana ambao wanaojishughulisha na masuala ya ufundi wa viyoyozi kwenye Majokofu ya mtumba kutumia aina ya gesi inayoruhusiwa na viwango vya kimataifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remidius Mwema akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema Dodoma inakuwa kwa kasi hivyo kuna haja ya kutengeneza jukwaa la pamoja litakalosaidia kutoa elimu kwa wananchi.

“Ni kweli wananchi wamekuwa wakinunua Majokofu ya mtumba ambayo yameonekana kuwa na madhara na hiyo yote inatokana na kutokuwa na uelewa juu ya madhara hayo lakini sasa kama tutakuwa na jukwaa la pamoja la kutoa elimu juu ya madhara ya bidhaa hizi za mtumba ninaimani bidhaa hizo za mtumba hazitanunuliwa,”amesema

Naye fundi anayejishughulisha na Ufundi wa Viyoyozi Matukuta Juma amesema kutokana na Ushauri huo   watahamasisha wengine kutumia mitungi ya gesi inayokubalika  huku akitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuwapunguzia gesi ambayo haiharibu mazingira kwani inauwza bei ya juu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com