Pasta wa kanisa moja kutoka eneo la Mitaboni, Machakos nchini Kenya amelazimika kuwahonga walevi kwa kuwanunulia pombe ili wasifichue siri yake ya kuwatongoza na kuchepuka na wake wa watu.
Penyenye zinasema kwamba mchungaji huyo anahudumu katika kanisa la kiroho lililoko sokoni na ana wafuasi wengi.
Kulingana na Taifa Leo, pasta anapokea hela nyingi za sadaka na matoleo mengine ambayo yamemfanya tajiri na kutokana na hilo alishindwa kustahimili majaribu ya mwili na anasa za dunia.
“Pasta alikuwa ndumilakuwili. Jumapili anajifanya mtakatifu kanisani na siku zingine alikuwa mtu wa dunia kiroho,” alisema mdaku.
Duru zinaarifu kwamba kando na pasta huyo kuchepuka na wake za watu alikuwa akibugia mvinyo kupindukia badala ya kujistahi kama tu aliyetarajiwa kuwa kielelezo chema katika jamii.
“Pasta alikuwa chui aliyevalia Ngozi ya kondoo. Alikuwa mhanyaji sugu na mlevi wa kupindukia,” mdaku alidokeza.
Hata hivyo, ilifika siku ambapo walevi walichoshwa na mienendo ya pasta ya kupita na wake za wenyewe bila kuona haya wala kujiheshimu.
Walevi hao walikata kauli kumkabili na kutisha kuanika uozo wake kwa waumini na pia kwa waume wa wanawake hao.
“Hata huoni haya kuchepuka na wanawake wa wenyewe kando na kwamba unabugia mvinyo bila kuogopa chochote? Hujui kuwa tunaweza kuanika siri zako kwa wat una upoteze heshima? Tabia yako mbaya sana na imetushinda!” mlevi mmoja aliwaka huku akimuingiza baridi mtumishi huyo.
Pasta alipohisi mambo yamekuwa mabaya alianza kuwasihi walevi hao. “Jameni msichome picha. Mimi ni binadamu kama nyinyi na nia hisia za kimwili pia. Semeni mnachotaka ili msinichafulie jina mitaani," pasta alisema.
Semasema zinaarifu kwamba walevi hao kwa kauli moja walimuamuru kuwanunulia pombe hadi watosheke naye akakubali huku akiwasihi wasijaribu kumuanika.
Hata hivyo baadhi yao baada ya kutosheka walisimama na kuanza kuondoka mmoja baada ya mwingine huku wakiimba nyimbo za kumsifu mchungaji huyo.
Duru zinaarifu kwamba pasta amekuwa kipenzi cha walevi hao na kila mara huwa anawanunulia dozi ili wasije wakaropoka na kumuanika.
Social Plugin