Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SEMA SINGIDA YAZINDUA MRADI WA KILIMO BIASHARA

Mkuu wa Wilaya ya  Manyoni Rahabu Mwagisa akizindua mpango wa uboreshaji wa maisha ya jamii kupitia mradi wa "Kilimo Biashara" unaosimamiwa na Shirika la SEMA mkoani Singida.


Na Edina Malekela,Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amesema Mkakati wa kitaifa wa kuondoa umaskini ni jukumu la Serikali,Sekta binafsi,Asasi zisizo za kiserikali (NGO'S) na washirika mbalimbali wa maendeleo ambapo unahitaji kuzingatia na kushughulikia kwa usahihi changamoto zinazowakabili wakulima wadogo.

Dkt. Mahange alisema hayo jana alipowakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa katika uzinduzi wa mpango wa uboreshaji wa maisha ya jamii kupitia mradi wa "Kilimo Biashara" unaosimamiwa na Shirika la SEMA mkoani Singida.

Alisema tafiti kadhaa zilizofanywa kuhusu umasikini zimebaini watu wengi masikini wanaishi vijijini na ni wakulima wadogo hivyo mikakati ya kitaifa ya kuondoa umasikini huo unahitaji kutatua kwa usahihi changamoto zinazowakabili wakulima hao.

Alisema mradi huo umeanza wakati muafaka ambapo mkoa kwa sasa unafikiria kuanzisha utekelezaji wa mpango wa kukuza uzalishaji wa zao la Alizeti unaolenga kuongeza uzalishaji wa mafuta yatokanayo na zao hilo kutoka tani 90,000 hadi tani 242,500 sawa na 54% ya jumla uagizaji wa mafuta hayo hapa nchini.

"Mpango huu wa uzalishaji utajumuisha washikadau wakiwemo wakulima wadogo,Vyama vya ushirika, Asasi za kiraia, wakulima wakubwa,Wizara ya Kilimo na Sekta binafsi." alisema na kuongeza.

"Matarajio yetu Mkoa na Wizara ya Kilimo katika utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa maisha ya jamii kupitia mradi wa Kilimo cha kibiashara ambao SEMA wanautekeleza utainua Uchumi wa wakulima wadogo wadogo kupitia kuongeza kwa tija ya mazao yatakayowezeshwa na mradi huu." alisema Dkt Mahenge.

Awali kabla ya kuzungumza Mkuu wa Mkoa Meneja Mkuu wa SEMA Ivo Manyaku alisema lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo wakulima waweze kujiunga kwenye vikundi vya kuweka na kukopa waweze kutunza mazao yao ili waje kuyauza kwa pamoja jambo litakalo wasaidia kuwa na sauti moja ya soko.

"Wakulima wengi wanauza mazao yao yakiwa shambani ili kukidhi mahitaji yao kutokana na kutokuwa na akiba hivyo ili wapate mahitaji wanayoyahitaji wanajikuta wanauza kwa bei ya hasara." alisema Manyaku.

Alisema kupitia mradi huo wanalenga kuyaongezea thamani mazao yanayozalishwa na wakulima,kuongeza mnyororo wa thamani ambapo mikakati ni kuwa na mashamba darasa,maonyesho ya Vijiji ya kibiashara ambapo watawaunganisha wasambazaji wa pembejeo ,maafisa Kilimo, wakulima na wanunuzi ili waone kila mmoja anahitaji nini jambo litakalosaidia mkulima kuwa na uhakika wa soko.

Meneja alisema mradi huo umewapa kipaumbele Wanawake na Vijana kwa zaidi ya 70% na utatekelezwa katika Wilaya tatu za mkoa huu ambazo ni Iramba, Ikungi na Manyoni huku ukitarajiwa kuboresha maisha ya wakulima wadogo 6,000 kwa kuimarisha miundombinu ya kusaidia biashara na mnyororo wa thamani wa mazao ya Mahindi,Mbaazi,Mtama pamoja na Alizeti.
Mkuu wa Wilaya ya  Manyoni Rahabu Mwagisa katikati  akiwa na viongozi wengine wakitembelea mabanda ya wajasiliamali kabla ya kuzindua mapanho wa uboreshaji wa maisha ya jamii kupitia mradi wa  kilimo biashara.

Meneja Mkuu wa SEMA Ivo Manyaku akizungumza kwenye ghafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya  Manyoni Rahabu Mwagisa akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com