Na George Binagi, Mwanza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuanzisha kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza ikiwa ni ubia baina ya shirika hilo na mwekezaji kampuni ya Rozella ya nchini Dubai.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Atupele Fredy Mwakibete alitoa pongezi hizo Septemba 12, 2021 baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichozinduliwa Juni 13, 2021 na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Alisema kiwanda hicho ambacho tayari kimeanza uzalishaji kitatoa mchango mkubwa katika soko la madini nchini kwa wachimbaji wa ndani na nje ya nchi kuuza madini yao na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta hiyo ya uchimbaji wa madini.
"Tumefurahishwa kuona bidii na juhudi za Wizara ya Madini kupitia shirika STAMICO kwa kuanzisha kiwanda hiki cha kipekee barani Afrika, tunaamini kitakuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji ndani na nje ya nchi kuleta dhahabu hapa", alisema Mwakibete.
Aidha Mwakibete alitoa wito kwa Wizara ya Madini kutafuta wabia wengine ili kuanzisha viwanda zaidi vya kusaga mchanga wenye madini/makinikia (Smelters) ili dhahabu inayopatikana isafishwe kwenye viwanda (Refineries) vya hapa nchini na hivyo kuzuia mwanya wa kusafirisha makinikia kwenda nje ya nchi.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukurani Manya alisema uwepo wa kiwanda hicho ni matokeo ya mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017 iliyotaka madini yote kuongezewa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi hivyo watanzania waanze kujivunia mabadiliko hayo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu ambavyo tayari vimejengwa Mwanza, Geita na Dodoma.
Prof. Manya alisema kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza kwa awali kitakuwa na uwezo wa kusafisha dhahabu kilo 480 kwa siku huku kikiwa na miundombinu ya kuongeza mitambo zaidi hadi kufika uwezo wa kusafisha kilo 960 kwa siku na hivyo kuwa kiwanda cha pili barani Afrika kikitanguliwa na kiwanda kilichopo Afrika Kusini chenye uwezo wa kusafisha kilo elfu moja kwa siku.
Kuhusu upatikanaji wa malighafi za kuendesha kiwanda hicho, Prof. Manya alisema jitihada mbalimbali za kuwezesha wachimbaji wadogo zinafanyika ili kuwasaidia wapate madini ya kutosha na kuyauza kwenye soko la madini lililopo kiwandani hapo huku akiongeza kuwa hivi karibuni mgodi mpya mkubwa wa Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema utaanza uzalishaji na kuchagiza zaidi malighafi kiwandani hapo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse aliwahimiza wachimbaji wote nchini, wakubwa kwa wadogo kuanza kupeleka madini yao kwenye kiwanda hicho ambapo watapata malipo yao kwa wakati na kwa bei shindani ya sokoni badala ya kupoteza muda kwa kuhangaika kuyapeleka nje ya nchi.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel aliahidi kushirikiana vyema na STAMICO ili kuhakikisha ulinzi na usalama vinaimarishwa kiwandani hapo ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuuza madini yao bila hofu huku pia akimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuhakikisha sekta ya uwekezaji inaendelea kuimarika na kuwavutia wawekezaji wengi hapa nchini.
Social Plugin