Naibu Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora Deogratius Ndejembi akiongea Kwenye uzinduzi wa mwongozo wa mapambano dhidi ya rushwa
Na Dotto Kwilasa - Dodoma
SERIKALI kupitia Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU)imezindua Muongozo wa Mkakati wa makubaliano baina yake na Chama cha Skauti Tanzania wenye lengo la kusisitiza ushirikishwaji wa wadau katika mapambano dhidi ya rushwa rushwa kuanzia ngazi ya chini.
Akiongea kwenye uzinduzi huo,Naibu Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora Deogratius Ndejembi amesema mwongozo huo utasaidia kujenga uchumi imara na kuchochea maendeleo ya huduma za kijamii.
Amesema Muongozo huo pia unajenga kuelimisha jamii kuacha vitendo vya rushwa huku akitoa maelekezo kwa maafisa elimu mikoa ,wilaya na maafisa TAKUKURU, kuhakikisha wanatenga muda wa kuelimisha vijana na jamii kwa ujumla kuhusu madhara ya rushwa.
Naibu Waziri Ndejembi amesema kutokana na kwamba vijana wengi wa Skauti wapo masomoni itakuwa rahisi kwao kufanya uelimishaji kupitia makundi mbalimbali huku akitoa agizo kwa wanufaika mafunzo hayo kupeleka kwa jamii elimu wanayoipata Kuhusu suala la rushwa.
Mbali na hayo ameeleza kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kuleta mafanikio ambayo yatafikisha ujumbe kimataifa kwamba Skauti ni kundi muhimu linaloshiriki kurudisha haki kwa kuzingatia uzalendo na uwajibikaji.
Kutokana na hayo,Skauti Mkuu Mwantumu Mahiza ametumia nafasi hiyo kuwataka Viongozi na Wakuu wa idara kuwapa ruhusa watumishi wa Umma kushiriki masuala ya Skauti pindi wanapohitajika na kuwapatia ruzuku Kwa ajili ya kujikimu Kwa kuwa kada hiyo haina fungu la ruzuku kwa wananchama wake.
Amefafanua kuwa,linapokuja Suala la Skauti kukutana ,baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Serikali wamekuwa wagumu kutoa ruhusa kwa wafanyakazi wao ambao ni wananchama wa Chama cha Skauti Tanzania kwa kisingizia cha kutokiwa na ruzuku jambo ambalo amesema linabomoa miiko na maadili ya utumishi wa Umma.
"Ziko baadhi ya Taasisi ambazo hadi sasa hazielewi wala kutilia maanani masuala ya skauti,kupitia hili naomba Serikali itoe mwongozo ili vijana wetu wa Skauti wasidharirike,Skauti sio uhuni,vijana hawa wana thamani ,wasomi na waadilifu lazima tuwaheshimu,"amesisitiza.
Mbali na hayo Skauti huyo Mkuu nchini,ameiomba serikali kuwaona vijana hao wa Skauti pindi linapokuja Suala la uteuzi wa Viongozi na kuihakikishia Serikali kuwa vijana hao ni waadilifu na wawajibikaji wasiopenda rushwa.
Skauti Mkuu Tanzania,Bi.Mwantumu Mahiza amesema mwongozo huo wa kufundishia masuala ya rushwa utakuwa na tija kubwa kwani vijana walio wengi hususan shuleni ndio waathirika wa rushwa kwa sababu rushwa huchelewesha maendeleo.
Aidha,amesema haiwezekani Tanzania tangu ipate uhuru mwaka 1961 bado inahangaika na miundombinu ya zahanati ,barabara kwani nchi zilizoendelea kuna masuala walishaacha na kujikita mambo mengine ya maendeleo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU Neema Mwakalyelye amesema mwaka 2019 walisaini mkataba wa makubaliano na chama cha Skauti Tanzania katika mapambano dhini ya rushwa na malengo ya mashirikiano hayo ni kuelimisha jamii madhara ya rushwa katika jamii .
Kupitia mkakati wa utekelezaji wa mwongozo huo,wanatarajia kuongeza upana wa makundi ya mapambano dhidi ya rushwa nchini ambapo kuna takriban vijana 105 wamenufaika na mafunzo hayo.
Mkurugenzi Elimu kwa Umma TAKUKURU Dkt. Emmanuel Kiyabo amesema mafunzo hayo yamehusisha wadau mbalimbali ikiwemo chama cha Maskauti Tanzania na watumishi kutoka TAKUKURU.
Social Plugin