WASICHANA WAVULIWA NGUO KISHA KUTEMBEZWA MTAANI WAKIWA UCHI NA CHURA


Wasichana sita wadogo katika eno la kati mwa India wamevuliwa nguo na kutembezwa katika maandamano wakiwa uchi kama sehemu ya matambiko ya kuombea mvua.

Tukio hilo lilitokea katika kijiji kilichokumbwa na ukame katika eneo la Bundelkhand jimbo la Madhya Prades.

Video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii inaripotiwa kuwaonesha wasichana wadogo wakitembea uchi wakiwa wamewekelea fimbo ya mbao iliyokuwa imefungwa chura mabegani.


Wakazi wanaamini matambiko hayo yanawatukuza miungu wa mvua kuleta mvua katika eneo hilo.

Tume ya Kitaifa ya kulinda na kutetea haki za watoto nchini India imeitisha ripoti kutoka kwa mamlaka ya Wilaya ya Damoh, ambako kijiji hicho kinapatikana.

Polisi wa Madhya Pradesh wamesema hawajapokea malalamiko ya aina yoyote dhidi ya hafla hiyo,lakini ameongeza kuwa wameanzisha uchunguzi.

"Hatua itachukuliwa endapo itabainika kuwa wasichana hao walilazimishwa kutembea uchi," Mkuu wa polisi wa Damoh Dkt. Teniwar aliambia shirika la habari Trust nchini India.

Video inaonesha wasichana hao, baadhi yao wana umri mdogo wa hadi miaka mitano,wakitembea katika maandamano hayo, wakifuatiwa na kundi la wanawake wanaoimba nyimbo za kidini.

Msafara huo ulisimama katika kila nyumba ya kijiji hicho huku watoto wakikusanya nafaka za chakula, ambazo baadaye zilitolewa kama msaada wa jamii katika hekalu la eneo hilo.

"Tunaamini hii italeta mvua," PTI aliwanukuu wanawake waliokuwa katika maandamano hayo wakisema.

Mratibu wa Wilaya ya Damoh S Krishna Chaitanya alisema wazazi wa wasichana hao walitoa idhini washiriki katika ibada hiyo.


"Katika visa kama hivyo, uongozi unaweza tu kuwafanya wanakijiji kuelewa athari za ushirikina huo na kuwafanya waelewe kuwa vitendo kama hivyo havileti matokeo yanayotarajiwa," akaongeza.


Kilimo cha India kinategemea sana mvua za masika na katika mikoa mingi, kuna matambiko yanayofanywa kuwatukuza miungu kulingana na mila na desturi za huko.


Baadhi ya jamii zinafanya yagnas (matambiko ya moto ya Kihindu), wengine wanabeba vyura au punda wakishiriki ibada hiyo huku wakiimba nyimbo za kuwatukuza miungu wa mvua.


Wakosoaji wanasema mila hiyo huwachanganya tu watu wa kawaida kutoka kwa ugumu, lakini wataalam wa kitamaduni wanasema mazoea hayo ni ishara ya kukata tamaa kwa wale ambao wanaamini kuwa hakuna mahali pengine pa kutafuta msaada.

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post