Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAUMINI WAPIGANA LIVE KANISANI


Mtu mmoja amejeruhiwa vibaya baada ya vurugu kuzuka wakati wa ibada katika kanisa la Kenya Assemblies of God, (KAG) eneo la Sagana kaunti ya Kirinyaga Jumapili, Septemba 19,2021

Imeripotiwa kwamba waumini walitaka Askofu Ben Irungu wa eneo la Mlima Kenya kuwatangazia mhubiri wao mpya ikizingatiwa wa awali alifariki dunia mwezi Machi mwaka huu.

 " Askofu, kabla ukamilishe ibada, tunafahamu leo ni siku kuu kwetu sisi kwa sababu unamtambulisha mhubiri mpya kufuatia kifo cha Mhubiri wa awali William Wachira ambaye aliaga dunia mwezi Machi mwaka huu," Muumini mmoja aliyetambulika kama Francis Gachau aliuliza. 

Waumini walimuidhinisha Mchungaji Esther Wachira ambaye alikuwa mkewe marehemu mchungaji Wachira.

“Huyu mama alianza kanisa na mume wake, sasa wakati Kanisa imesimama wanataka kupatia mtu mwingine uongozi wa kanisa, hatutakubali hilo,” Baadhi ya waumini walisema. 

Waumini walimkashifu Askofu Irungu kwa kupendekeza mhubiri Nahashon Maina ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu pasta Wachira. 

"Tulifunga na kuomba kwa siku 21 na tukaamua ni mchungaji Esther Wachira atakayeliongoza kanisa, na sasa wanataka kumtawaza pasta Maina, jambo hilo halitakubalika hata kidogo," Shemasi wa kanisa hilo alisema.

Pindi tu baada ya shemasi huyo kumaliza kutoa matamshi hayo, vurugu ilizuka huku waumini wakigombana na katika harakati hiyo mmoja wa waumini aliyetambulika kama Gachau alipigwa na kujeruhiwa. Akizungumza na wanahabari, Gachau alimkashifu Pasta Maina kwa kumpiga kichwani kwa kutumia kipaza sauti na kumuacha akivuja damu.

 “Pasta Maina ndiye amenigonga, mimi nilikuwa nasimama kuuliza swali tu akaniumiza, hata kama nitauawa, sisi tunataka Mchungaji Esther Wachira,” Gachau alisema. 

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Sagana walifika katika kanisa hilo na kutuliza hali, waumini waliamrishwa kuondoka mara moja.

Afisa mkuu wa polisi eneo la Sagana amesema viongozi wote wa kanisa hilo watatarajiwa kufika kituoni kuelezea kilichojiri.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com