Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo (katikati) akikabidhi kiti mwendo kwa mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge mara baada ya kupokea vitaa tiba toka taasisi ya Doris Mollel Foudation, kulia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Doris Mollel foundation Doris Mollel.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo (katikati) akipokea moja ya mashuka kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Maswa, msaada mabao umetolewa na taasisi ya Doris Mollel Foundation, kushoto ni Mkurugenzi wa taaisisi hiyo ya Doris Mollel bi, Doris Mollel na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo (mwenye suti ya kijivu) akikabidhi mashine ya kusaga unga lishe kwa mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge mara baada ya kutolewa na taasisi ya Doris Mollel Foundation, kulia na kushoto ni baadhi ya madiwani waliofika kushuhudia tukio hilo. (Picha na Costantine Mathias)
***
Na Costantine Mathias- Maswa.
MBUNGE wa jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo amepokea vifaa tiba mbalimbali vya matibabu kwa niaba ya wananchi vinavyolenga kuokoa maisha ya watoto njiti katika hospitali ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Vifaa hivyo vimetolewa na Doris Mollel Foundation na kukabidhiwa mbunge huyo katika sherehe fupi iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wananchi wa wilaya hiyo.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya umri ni pamoja na Mashine 3 za kupumulia,Vitanda 6 vya kisasa vya wagonjwa, Magodoro 30, Mashuka 100 na Baiskeli 7 za miguu mitatu kwa wagonjwa.
Vifaa vingine ni pamoja na mashine ndogo mbili za kusagia nafaka kwa ajili ya watoto hao na wazazi wao wanapokuwa wakipata matibabu hospitalini hapo, Seti tatu za runinga zilizotolewa na DSTV ambazo zitafungwa katika wodi ya kulazwa watoto hao na vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 50.
Mkurugenzi wa mfuko wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel alisema kuwa anaguswa na maisha ya watoto hao kutokana na yeye mwenyewe kuwa mhanga wa tatizo hilo alipozaliwa na kufanikiwa kukua katika afya salama anatambua changamoto wanazokumbana nazo watoto hao katika ukuaji na hivyo kuguswa na kutoa misaada hiyo.
"Mimi nimeguswa na maisha ya watoto hawa wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda wa miezi tisa(watoto njiti)kutokana na mimi kuzaliwa katika hali hiyo hivyo nilisimuliwa na wazazi wangu na nililewa vizuri kwa kupata huduma nzuri ndiyo maana nimeguswa sasa kuwasaidia watoto hao kwa kutoa misaada mbalimbali ili kunusuru maisha yao,"alisema.
Akipokea vifaa hivyo Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo pamoja na kumshukuru Doris Mollel Foundation na washirika wake kwa kutoa misaada hiyo kwa ajili ya kuwanusuru watoto hao alisema kuwa vifaa hivyo atavikabidhi kwa Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Maswa na kuwekwa kwenye wodi mpya ya watoto watakaozaliwa wakiwa katika hali hiyo.
Alisema kuwa kwa sasa watoto njiti watakaozaliwa katika wilaya hiyo hawatapelekwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza kwani watapata huduma hiyo katika hospitali hiyo ya wilaya.
"Watoto watakaozaliwa njiti katika wilaya yetu na hata mkoa mzima wa Simiyu watapatiwa matibabu hapa hapa kwenye hospitali ya wilaya ya Maswa na hawatapelekwa tena kwenye hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliyoko jijini Mwanza,"alisema.
Alisema kuwa gharama ya kuwalea watoto hao ni kubwa hivyo ni vizuri wananchi wa wilaya hiyo na mkoa mzima wa Simiyu wakaitumia huduma hiyo ambayo kwa sasa imesogezwa karibu.
Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye alipokea vifaa hivyo kutoka kwa mbunge huyo alimpongeza kwa kazi kubwa anazozifanya katika jimbo la kuwaletea wananchi maendeleo sambamba ya kujali afya zao kwa kutafuta wafadhili kwa ajili ya afya za wapiga kura wake.
"Mimi nikupongeze Mbunge kwa kazi nzuri unazozifanya za kuwatumikia wananchi wa jimbo lako na leo tumeona umeleta wafadhili hawa Doris Mollel Foundation na washirika wake wametupatia vifaa hivyo vya matibabu kwa watoto njiti katika hospitali yetu ya wilaya tunashukuru kwa kutusogezea huduma hii muhimu sana kwa watoto hao,"alisema.
Social Plugin