Na. Sandra Charles, Regina Frank na Rahma Taratibu, SJMC, Dodoma
Asasi za kiraia na za kidini zimeahidi kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kwa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ili kuchochea maendeleo nchini.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Dodoma na Asasi za Kiraia na Asasi za Kidini wakati wa mkutano kati ya asasi hizo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), mkutano ulioangazia ushiriki wa asasi hizo katika maendeleo ya Taifa.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa alisema kuwa Asasi za kiraia zimekuwa wadau wakubwa katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya sekta za maendeleo, ikiwemo ya elimu na Afya.
“Tumewasilisha rasmi mpango wa utekelezaji na ushiriki wa asasi za kiraia katika mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa na pia kujenga makubaliano ya pamoja na Serikali kuhusu namna ya kutekeleza mpango huo”, alisema Bw. Olengurumwa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Haki, Amani na Uadilifu wa uumbaji, Dkt. Camillius Kassala, alishauri vijana kuletwa pamoja kwa kujiunga katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa wanaohitimu Kitato cha sita ili kupunguza changamoto mbalimbali zikiwemo za kimaadili katika jamii na kujenga uzalendo.
Naye, Mwenyekiti wa Asasi ya Kiraia ya Women Wake Up (WOWAP) Dodoma, ambaye pia ni Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Fatma Hassan Toufiq, alisema kuwa Asasi za Kiraia hukusanya michango kutoka vyanzo mbalimbali hivyo ni vema Serikali ikajua namna zinavyofanya kazi lakini pia akaiomba Serikali itenge bajeti kwa asasi za kiraia ili kuziwezesha kutekeleza majukumu mbalimbali kwa jamii badala ya kutegemea wafadhili katika kuchochea maendeleo nchini.
Vilevile Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Bw. Nuhu Jabiri Mruma, alisema kuungana kwa Asasi za kiraia, Kidini na Serikali kutakuwa na tija katika kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa hivyo kuendeleza uchumi wa jamii, mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema kuwa ni vema makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia yakawekwa wazi ili kujua wahusika wakuu katika ushirika huo lakini pia mawanda yake na namna ya mapitio ya ajenda mbalimbali.
Aidha amezipongeza Asasi za Kiraia kwa kuonesha nia thabiti ya kushirikiana na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango na Asasi za Kiraia na za Kidini umefanyika kwa mara ya kwanza hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Asasi hizo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mwisho
Tags:
habari