CHADEMA WASHAURIWA KUWEKA PICHA YA RAIS KWENYE OFISI ZAO



Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeishauri CHADEMA kuweka picha ya Rais katika ofisi za viongozi wa chama hicho kwa sababu hiyo ni taasisi ya umma.

Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Septemba 10, 2021 na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza wakati wakifanya ukaguzi wa chama hicho katika utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Amesema ofisi za vyama vya siasa ni ofisi za umma hivyo ni vizuri wakaendeleza utamaduni wa kuwa na picha ya Rais kwenye taasisi za umma.

“Hii ni ofisi ya umma, ni vizuri kukawa na picha ya Rais ukutani, siyo unaweka picha ya katibu mkuu. Huu ni ushauri tumewapa, tutapita Januari kuona kama wamelifanyia kazi,” amesema Nyahoza.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA – Zanzibar, Salum Mwalimu amesema Msajili amekuta mambo yamekaa vizuri ndiyo maana akagundua hakuna picha ya Rais.

“Tumempokea Msajili, wamepitia taarifa zote walizozihitaji wamekuta mambo yako vizuri, ni masuala madogo madogo ndiyo yanahitaji kufanyiwa kazi. Kama angekuta mambo makubwa, asingekumbuka kuangalia picha ya Rais,” amesema Mwalimu.

Ofisi ya Msajili inaendelea na ukaguzi wa vyama vya siasa na leo walikuwa wakikagua Chadema ambapo Nyahoza amesema wamefurahishwa na mfumo mzuri wa uwekaji kumbukumbu za fedha na wana mfumo mzuri wa utawala.

Hata hivyo, amesema wamebaini mapungufu kadhaa ikiwemo uwekaji kumbukumbu kwenye mali za chama na pia wameanza kutumia bajeti ambayo wameiandaa lakini haijaidhinishwa na kamati kuu kama katiba yao inavyotaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post