TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIDHINISHWA
KWA FEDHA ZA MKOPO NAFUU WA KUKABILIANA NA ATHARI ZA UVIKO-19 KUTOKA IMF
Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba kupitia dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) wa jumla ya dola za Marekani milioni 189.08; na mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI) wa dola za Marekani milioni 378.17.
Fedha hizo zitatumika ndani ya mwaka huu wa fedha katika kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na UVIKO-19.
Sekta zitakazonufaika kulingana na makubaliano yetu na IMF ni afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya maskini kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii (TASAF) na kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Kila sekta itatumia fedha hizo kwenye masuala yanayolenga kukabiliana na na athari za UVIKO-19 ambapo pamoja na mambo mengine, Sekta ya afya itanunua dawa na vifaa tiba vya kupambana na UVIKO-19 na kugharamia utekelezaji wa mpango wa chanjo.
Sekta ya elimu itaweka mazingira yatakayowezesha wanafunzi kujifunza bila msongamano na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maboma ya shule na kuongeza madawati.
Sekta ya maji itaongeza miundombinu ya maji itakayowezesha upatikanaji wa huduma ya maji tiririka kwa wingi zaidi mijini na vijijini; na Mpango unaoendelea wa TASAF utaongezewa fedha (Complement) ili kusaidia kaya maskini zilizoathirika na UVIKO 19.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itawezeshwa pia kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta zilizoathirika ikiwa ni pamoja na afya, utalii na kilimo.
Waziri mwenye dhamana ya Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameziasa sekta zote zitakazopata
fedha hizi kuzitumia kulingana na Mpango tulioandaa kwa pamoja na sekta husika
wa kukabiliana na athari za UVIKO-19 – Tanzania
COVID-19 Socio-Economic Recovery and Response Plan (TCRP). Aidha, fedha
hizo zitumike kwa kuzingatia makubaliano yetu na IMF kama ilivyoainishwa kwenye
barua ya dhamira ya Serikali (Letter of Intent - LOI) ikiwa ni pamoja na utoaji
wa taarifa za utekelezaji kwa wakati.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO