Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC) ,Peter Maduki akizungumza na waandishi wa habari kwenye Mkutano Mkuu wa 84 wa Mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) unaofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya kutoka Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC) Dkt.Josephine Balati,akizungumza na waandishi wa habari kwenye Mkutano Mkuu wa 84 wa Mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) unaofanyika Jijini Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC) ,Peter Maduki akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kwenye Mkutano Mkuu wa 84 wa Mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) unaofanyika Jijini Dodoma.
.................................................................................
Na.Alex Sonna,Dodoma
TUME ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC) imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kuharakisha mchakato wa bima ya afya kwa wote ili kila mtanzania aweze kupata matibabu ya uhakika pindi anapoumwa.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo,Peter Maduki alipokuwa akizungumza kwenye mkutano Mkuu wa 84 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA).
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa CSSC ametoa rai kwa Serikali itekeleze haraka mchakato huo wa bima kwa wote ili kila mtanzania aweze kupata matibabu ya uhakika pindi anapoumwa.
“Ili wananchi wote waweze kupata huduma bora tunaiomba Serikali itekeleze bima ya afya kwa wote mara moja ili kusudi watoto, watu wazima na kina mama na watu wote waweze kunufaika,”amesema.
Aidha, Maduki amewahamasisha watanzania kujiunga na bima ya afya kuanzia ile ya jamii na Taifa ili waweze kupata huduma.
“Nawahamasisha wananchi waweze kujiunga na bima ya afya kuanzia ngazi mbalimbali kuanzia ile ya ngazi ya jamii na ile ya taifa kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati,”amesema.
Amesema wao kama Kanisa wanaendelea kuwaelimisha watanzania kuendelea kupata chanjo ya Uvico -19 ndio maana wameandaa mafunzo kwa wataalamu wa afya, jinsi ya kujikinga pamoja na kutoa vifaa(PPE) ambavyo wamevigawa katika Hospitali 200 nchini.
“Kama Kanisa tunapendekeza kwamba watu waweze kupata chanjo ndio maana sisi kama Kanisa tumehakikisha tunatoa mafunzo kwa wataalamu wa afya waweze kujikinga pia tumehakikisha tunapata vifaa vya kutosha kutoka kwa wadau wetu na kuvigawa katika Hospitali zetu zipatazo takribani 200,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema wameendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wa Dini ili wawe na uelewa na kisha wawaelimishe waumini.
Mkurugenzi huo Mtendaji amesema katika mkutano huo watazungumzia namna bora ya kuboresha sekta ya afya,elimu pamoja na kuhamasisha matumizi ya bima ya afya ili watanzania wengi waweze kupata huduma pindi wanapoumwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Afya kutoka Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC)Dkt.Josephine Balati amesema Taasisi ya CSSC inajishughulisha na utoaji wa huduma za afya na elimu ambazo zinatolewa na Makanisa nchini ambapo amedai wanafanya kazi na taasisi zaidi ya 900 ambazo zipo sehemu mbalimbali hapa nchini.
“Sisi ambao tunafanya kazi na hizi taasisi za Dini tunashirikiana sana na Serikali yetu.Katika chanjo tunashiriki kikamilifu kuielimisha jamii kuchanja tunajua ukubwa wa tatizo hili kwa hiyo tunaendelea kuihamasisha jamii kuchanja.Sisi tumeshirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi,”amesema.
Amesema suala la elimu bado linahitajika ambapo kwa kupitia Taasisi zao wameendelea kuwahamasisha viongozi wa Dini pamoja na kuwajengea uwezo ili jamii ione umuhimu wa kuchanja.
“Tuna redio za makanisa na viongozi wa Dini tunawataka kuendelea kutoa elimu na sisi tunawajengea uwezo ili waweze kuelimisha, suala la elimu ni muhimu sana katika jamii,”amesema