Na Dotto Mwaibale, Mkalama
WAFUGAJI wilayani Mkalama mkoani Singida wametakiwa Kufuga kwa tija na kisasa ili kuweza kunufaika na ufugaji wao kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo juzi wakati akihitimisha zoezi la chanjo ya mifugo dhidi ya ugonjwa wa Kimeta Chambavu kwa Ng'ombe na minyoo ya aina mbalimbali kwa mbuzi na kondoo katika Kijiji cha Kisuluiga Kata ya Gumanga.
Kizigo amezitaka familia na wafugaji kuitumia vizuri mifugo yao kwa kujenga nyumba za kisasa na kuondoa nyumba za tembe ambazo bado zipo chache.
Aidha amewataka wananchi kuona umuhimu wa kuchanja mifugo yao kwani kwakufanya hivyo kutapunguza hasara kwa wafugaji na kunufaika na mifugo yao na ili waweze kupata soko zuri ni lazima mifugo iwe na afya njema na kuwataka kutumia zoezi hili la Kikatiba kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao kwani ufugaji wenye tija ni ule unaolenga kuongeza ubora wa mazao yatokanayo na mifugo na kumnufaisha mfugaji ili kukuza pato la familia, jamii na nchi kwa ujumla.
" Nawasihi wafugaji mfuge kwa tija kwa maendeleo endelevu na ustawi wa jamii ,sitegemii mfugaji ana ng'ombe 20 lakini analala kwenye nyumba ya Tembe au watoto wake wanalala njaa ni kitu ambacho hakiwezekani" alisema Kizigo.
Awali akisoma Risala kwa mgeni Rasmi Kaimu Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dotto Michael alisema kuwa pamoja na changamoto zinazoikali idara hiyo wamefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na mifugo kutoka 22% mwaka 2O13 hadi 5% mwaka 2O2O huku akitaja juhudi hizo zinatokana na halmashauri kushirikiana na Idara na wanategemea kupunguza zaidi ya hapo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama ambaye ni Diwani wa Kata ya Gumanga James Mkwega ameishukuru Serikali kwa juhudi za kupambana na ugonjwa wa mlipuko kwa mifugo ambao hapo awali ulisababishia hasara kwa wafugaji wengi na kusema kuwa watatumia fursa hiyo ya kikatiba kuchanja mifugo yao na kufuga kwa tija kwa masilahi ya jamii ya Mkalama.
Baadhi ya wafugaji Bakari Msilau na Lea Gunda wamesema kuwa pamoja na kuitikia wito wa kuchanja mifugo wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya majosho kwa ajili ya kuogesha mifugo yao pamoja.
Social Plugin