Mapokezi ya Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Said, alipowasili rasmi Makao Makuu ya Ofisi hizo Dodoma, Septemba 29, 2021.
Mkurugenzi mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Said akipokea shada la maua kutoka kwa mfanyakazi wa REA, Eshimuni James, alipowasili rasmi Makao Makuu ya Ofisi hizo Dodoma, Septemba 29, 2021.
Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiimba wimbo wa ‘Mshikamano Daima’ wakati wa hafla fupi ya kumpokea Mkurugenzi mpya wa REA, Mhandisi Hassan Said na kumwaga Mtangulizi wake Mhandisi Amos Maganga (hawapo pichani), Septemba 29, 2021 Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Said (wa tatu-kulia) na Mtangulizi wake, Mhandisi Amos Maganga (wa tatu-kushoto) baada ya makabidhiano rasmi ya Ofisi Septemba 29, 2021 Dosoma. Wengine pichani ni baadhi ya Wajumbe wa Bodi.
Mhandisi Amos Maganga akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) – (hawapo pichani), baada ya kukabidhi rasmi Ofisi kwa Mkurugenzi mpya wa REA, Mhandisi Hassan Said, Septemba 29, 2021 Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (kulia), akimtambulisha rasmi Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said kwa Wafanyakazi wa REA mara baada ya kukabidhiwa rasmi Ofisi, Septemba 29, 2021 Dodoma.
Mkurugenzi mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said akizungumza na wafanyakazi wa REA baada ya kukabidhiwa rasmi Ofisi na Mtangulizi wake Mhandisi Amos Maganga, Septemba 29, 2021 Dodoma.
Mkurugenzi mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said (kulia) akipokea Kabrasha lenye taarifa mbalimbali kuhusu REA kutoka kwa Mtangulizi wake, Mhandisi Amos Maganga katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi, Dodoma, Septemba 29, 2021.
*************************
Na Veronica Simba - REA
Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amekabidhiwa rasmi Ofisi na Mtangulizi wake, Mhandisi Amos Maganga leo Oktoba 29, 2021 ambapo amewaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu.
Mhandisi Said amesema matumaini ya Watanzania, hasa wa vijijini, yanategemea dhamana ambayo REA imepewa.
“Tukitetereka katika kutimiza majukumu yetu, tutafifisha matumaini ya Watanzania wengi ambao wanategemea nishati kama nyenzo ya kubadilisha maisha yao,” amesisitiza.
Aidha, Mkurugenzi huyo mpya wa REA amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini kuwatumikia Watanzania katika wadhifa huo na kuahidi kuwa hatamwangusha.
Vilevile, ametoa pongezi kwa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) chini ya Mwenyekiti Wakili Julius Kalolo, Mtangulizi wake Mhandisi Maganga pamoja na wafanyakazi wote wa REA kwa kazi nzuri iliyofanyika na kufikia hatua nzuri katika kusambaza nishati vijijini.
“REA ni miongoni mwa Taasisi za Umma ambazo zimefanya kazi kubwa sana na ambazo zimegusa maisha ya wananchi. Huwezi kupata mafanikio kama haya ikiwa hauna Bodi imara na yenye weledi mkubwa, Menejimenti nzuri na wafanyakazi wanaojituma,” amefafanua.
Sambamba na hayo, Mhandisi Said ameomba ushirikiano kutoka kwa Bodi, Menejimenti na Watumishi wote wa REA katika kutekeleza majukumu yake.
Awali, akizungumza baada ya kukabidhi rasmi Ofisi kwa Mkurugenzi mpya, Mtangulizi wake Mhandisi Maganga amemshukuru Mungu, Bodi na Wafanyakazi wote wa REA kwa kumpatia ushirikiano katika kipindi chote alichofanya kazi nao.
Mhandisi Maganga amebainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya nishati vijijini, yanatokana na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwao.
Amewataka kumpatia ushirikiano wa aina hiyo, Mkurugenzi mpya huku akibainisha kuwa yeye binafsi anamwamini na anamtambua kama mchapakazi na mwenye uhodari katika utendaji kazi.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti Wakili Julius Kalolo amempongeza Mhandisi Hassan kwa kuaminiwa na Rais na kuteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa. Amemwahidi kuwa Bodi itampatia ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, amempongeza na kumshukuru Mhandisi Maganga kwa ushirikiano alioutoa kwa Bodi katika kipindi chote alichofanya kazi katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu.
Aidha, wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya Menejimenti ya REA na wafanyakazi wote, Kaimu Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti, Mhandisi Elineema Mkumbo, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Grace Sengula pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Tawi la REA, Swalehe Kibwana, wameahidi ushirikiano pamoja na kutekeleza yale yote aliyoyasisitiza Mkurugenzi mpya.
Mhandisi Hassan Said aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa REA kuanzia Septemba 23 mwaka huu akitokea Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) alikokuwa akifanya kazi kama Meneja Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki.
Social Plugin