Prisca Ulomi na Faraja Mpina, Dodoma
Mbunge wa Kigamboni na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile leo tarehe 20.09.2021 amekabidhi rasmi Ofisi kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa fursa ya kuhudumu katika Wizara hiyo katika kipindi cha miezi sita ya Serikali ya Awamu ya Sita
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na Menejimenti ya Wizara hiyo Dkt. Ndugulile amempongeza Dkt. Kijaji kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo na kumzungumzia kuwa ni kiongozi makini, mwenye uwezo mkubwa na anaamini atakuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA
Aidha, Dkt. Ndugulile ameishukuru Menejimenti ya Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kufanya kazi ya kuijenga Wizara hiyo na hatimaye kuongezewa majukumu mengine huku akiyataja baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara, mabadiliko ya Sheria mbalimbali, kuboresha utendaji wa taasisi na kukamilisha muundo wa Wizara
Dkt. Ndugulile amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuendeleza mazuri yaliyofanyika na kwa nguvu ileile waendelee kutekeleza mazuri mengi zaidi kwa kushirikiana kwa karibu na Dkt. Kijaji kwa kuwa anaondoka katika Wizara hiyo akiwa ameiacha katika mikono salama
Naye Dkt. Kijaji amemshukuru na kumpongeza Dkt. Faustine Ndugulile kwa kuweka misingi imara katika Wizara hiyo na kufahamika kwa majukumu inayotekeleza kwa kuhakikisha watendaji wa Wizara hiyo na taasisi zake wanashirikiana kwa karibu katika kuwahudumia wananchi
Amesema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani alimuamini Dkt. Ndugulile kuendelea kuiongoza Wizara hiyo hivyo anapokea Wizara hiyo huku akiamini kuwa kulikuwa na mtu imara aliyetengeneza mazingira mazuri ya kuendelea kutoa huduma bora za Habari, Mawasiliano na TEHAMA kwa wananchi
Aidha, amemtaka Dkt. Ndugulile asifunge milango kwa sababu bado ni mdau mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kupitia utendaji wa Wizara hiyo mtambuka na wezeshi kwa Wizara na taasisi za Serikali katika kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa pamoja kupitia huduma za mawasiliano na TEHAMA
“Sisi wote ni watanzania lengo letu ni kuijenga Tanzania hivyo uzalendo wetu, upendo wetu pasipo chuki na umoja wetu ndio kitakachofanikisha kutimiza malengo tuliyojiwekea”, amezungumza Dkt. Kijaji
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa utumishi wake na kumkaribisha rasmi Waziri wa Wizara mpya ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji na kumuahidi ushirikiano mkubwa katika kuendelea kutimiza majukumu yaliyo mbele yake ya Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zikiwemo taasisi mbili zilizo chini ya Sekta ya Habari ambazo ni Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa kuna tofauti kubwa iliyoonekana tangu Wizara hiyo ikiwa Sekta mpaka mabadiliko yaliyoonekana kwa kipindi cha miezi 9 na Menejimenti hiyo imejifunza mengi kupitia kwake ikiwa ni umoja, amani, upendo na mshikamano na atakaoenda kukutana nao aendelee kuwa zawadi kwao
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Social Plugin