Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KITUO CHA UVUVI KUJENGWA KAGERA

Viongozi Wakuu kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakitia saini katika mkataba wa makubaliano ya kujenga Kituo  cha umahiri katika utafiti na ubunifu kwenye uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji mkoani Kagera juzi. Wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania(TACT), Dkt. John Kyaruzi, na wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah. Wa kwanza kutoka kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Profesa. Emmanuel Luoga na wa Pili kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa. Faustine Kamuzora.

    Viongozi Wakuu kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakionesha mkataba wa makubaliano muda mfupi baada kutia  saini ili  kujenga Kituo  cha umahiri katika utafiti na ubunifu kwenye uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji mkoani Kagera juzi. Wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania (TACT), Dkt. John Kyaruzi, na wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah. Wa kwanza kutoka kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Profesa. Emmanuel Luoga na wa Pili kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa. Faustine Kamuzora.  


Na Mbaraka Kambona, Kagera

 

Serikali kupitia Sekta ya Uvuvi imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania (TACT) na Serikali ya Mkoa wa Kagera ili kujenga Kituo cha Umahiri na ubunifu katika Uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto za utafiti, ugani na ubunifu ili kuongeza tija katika Sekta hiyo nchini. 

Akizungumza wakati akifungua hafla fupi ya utiaji saini katika mkataba wa makubaliano hayo juzi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali, Charles Mbuge aliwataka viongozi wa mkoa huo kuupokea mradi huo akisema kuwa hiyo ni neema iliyowafikia katika mkoa wao. 

"Halmashauri zetu mpo hapa pamoja na viongozi, naomba suala hili mlitilie maanani, uwekezaji huu ukifanikiwa hapa kwetu utasaidia kujenga uchumi wa mwananchi mmoja mmoja hadi Taifa kwa ujumla," alisema  Meja Jenerali Mbuge. 

Alisema kuwa viongozi hao hawana budi kukusimamia mradi huo  unafanikiwa ili uweze kuleta tija kwa jamii hususani vijana waweze kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na kukuza uchumi wao na wa nchi pia. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kutasaidia kutatua changamoto nyingi zinazokabili sekta ya Uvuvi na tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji. 

"Napenda kuwaahidi wadau wote wa sekta ya uvuvi kuwa wizara yangu itaendelea kuunga mkono juhudi za wavuvi, wakuzaji Viumbe Maji, Wachakataji na Wafanyabiashara wa bidhaa za Uvuvi ili ziweze kuwa na tija na kuleta ustawi wa wadau wote nchini,"  alisema Dkt. Tamatamah. 

Naye, Mkurugenzi Mtendaji, Mfuko Kichocheo wa Kilimo Tanzania, Dkt. John Kyaruzi alisema kuwa  wameamua kuwekeza katika utafiti kwenye Sekta ya uvuvi ili iweze kuwa endelevu na kuwasaidia wawekezaji kuwa na taarifa za msingi zitakazowasaidia kuwekeza kwa tija ili kuimarisha biashara zao. 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Profesa. Emmanuel Luoga alisisitiza kuwa nia ya chuo chake ni kufanya tafiti zitakazotoa matokeo chanya kiuchumi na kiikolojia ili kufanya shughuli za uvuvi kuwa endelevu. 

Katika sehemu ya makubaliano hayo Wizara imepanga kufanya tathmini ya  mazingira na kurekebisha sera na sheria zote ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa kikwazo kwa shughuli za uvuvi, Serikali ya mkoa imetoa eneo kwa ajili ya kufanya uwekezaji huo wa mradi, Chuo Cha Nelson Mandela kitajikita kufanya tafiti tumizi ili kusaidia Sekta ya Uvuvi na wadau wake kuwa na taarifa sahihi zitazowasaidia kuboresha shughuli zao na Mfuko Kichocheo wa Kilimo (TACT) watawekeza mitaji ili kuchachua uwekezaji katika Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji nchini. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com