Wanamuziki Hafsa Kazinje, Kunukura Elibariki na Komandoo Hamza Kalala (kulia) wakitoa burudani ndani ya Hoteli ya Kitalii ya Kibo Palace jijini Arusha jana ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Muziki Duniani yanayofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Na Dotto Mwaibale, Arusha.
WANAMUZIKI Komandoo Hamza Kalala, Hafsa Kazinje na Kunukura Elibariki wamewasha moto kwa kutoa burudani ya aina yake Hoteli ya Kitalii ya Kibo Palace jijini Arusha na kuwafanya Mkurugenzi wa jiji hilo Dkt.John Pima na Meya wake Maximilian Iranghe wakishindwa kuvumilia kutokana na midundo nakujikuta wakipanda jukwaani kuserebuka.
Burudani hiyo ya aina yake ilitolewa na wanamuzi hao jana ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Muziki Duniani yanayofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini ambayo yalizinduliwa mwanzoni mwa wiki Makumbusho ya Kihistoria ya Taifa jijini hapa kwa kuandaliwa na Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) ambayo kilele chake ni Oktoba 1, 2021
Katibu Mkuu Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel akimkaribisha Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt.John Pima ili aseme chochote wakati burudani hiyo iliyoandaliwa na jiji hilo kwa kushirikiana na TAMUFO alisema mwezi huu wote utakuwa na shughuli mbalimbali zitakazo fanywa katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha shughuli za maendeleo na kutanga vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Arusha.
Alisema maadhimisho hayo yanakwenda sanjari na kauli mbiu isemayo Muziki ni Kazi Fahari na Urithi wa Utamaduni Wetu.
Joel alisema Wanamuziki wa kada zote katika maeneo mbalimbali watashiriki kuhamasisha shughuli hizo kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.
Joel alitumia nafasi hiyo kutoa shukurani kwa Serikali ya Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya jiji hilo kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika kuadhimisha maadhimisho hayo ya kihistoria hapa nchini ambapo Mkoa wa Arusha ni mwenyeji.
Alisema wamechagua Jiji la Arusha kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo Kimataifa kwa sababu Mkoa wa Arusha ni Mkoa wa Kitalii ambao unaliingizia taifa mapato mengi kupitia sekta hiyo na upo katikati ya Afrika pia una Historia kubwa ya nchi yetu ambapo Mhasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Azimio la Arusha katika mkoa huo na alitembea kwa miguu na viongozi wengine kuunga azimio hilo na kuwa Arusha ndipo kilipo kiti na mti wa Mwalimu Nyerere.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima alisema katika mwezi huu kuelekea kwenye kilele chenyewe kutakuwa na shughuli mbalimbali na kuonesha kazi na fani za wadau na kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya jiji hilo na kuwa wataendelea kushirikiana na TAMUFO na kuwa burudani hiyo ya muziki ni ya kwanza kwani kuna matukio mengine mengi yataendelea kufanyika.
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranghe alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujitokeza hadharani kuchanja chanjo ya Uviko kwani baada ya kuchanja tu makundi ya watalii yalianza kuingia Arusha kwa wingi na kuufanya mzunguko wa fedha uliosimama kuanza upya.
Meya Iranghe aliwakaribisha wageni wote walioungana na viongozi wa jiji hilo katika burudani hiyo ya kipekee na akawapongeza wanamuzi hao kwa kutoa burudani safi ambayo imewatendea haki wana Arusha na TAMUFO.
Diwani wa Kata ya Sakei Gerald Sebastian alimuomba Meya na Mkurugenzi wa jiji hilo kufungua burudani zilizosimama ili kuruhusu mzunguko wa fedha na maadhimisho haya yawe chachu ya kufungua burudani hizo.
Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara Kamishna Msaidizi Mwandamizi Dkt. Noelia Myonga aliwakaribisha wananchi kutembelea hifadhi za taifa kwani gharama zake ni ndogo kila mtu anaweza kuzimudu.
"Jamani tuna hifadhi za Manyara, Tarangire, Mkomazi na Kilimanjaro njooni mzitembelee ili mzitangaze kwa watanzania kwa mtu mmoja ni Sh.11,800 tu na ukija na gari lako ni Sh.23,600 na ukitaka mtu wa kukutembeza utalipa Sh.5000 na kuna wapishi wazuri ambapo mtapata maanjumati karibuni sana," alisema Myonga.
Mlezi wa TAMUFO Frank Richard alisema burudani hizo kwa mwezi mzima zitaendelea kufanyika katika Hoteli ya Kitalii ya Kibo Palace zikisindikizwa na vinywaji, vyakula mbalimbali na nyama choma ilinayoandaliwa na wachomaji mahiri wa hoteli hiyo huku wakipatiwa huduma na wahudumu warembo wenye mvuto na uzoefu mkubwa wa kuhudumia wateja.
Mwanamuziki Mahiri wa Miondoko ya Zuku Tanzania na mwimbaji wa nyimbo za injili aliyetamba na kibao chake cha presha Hafsa Kazinja,Komandoo Hamza Kalala na Kunukura Elibariki walitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi katika kilele cha siku hiyo ya maadhimisho ya kitaifa yatakayofanyika Oktoba 1, 2021ili wapate burudani kutoka kada ya wanamuziki mbalimbali kwani siku hiyo jiji hilo litawaka moto kutokana na burudani safi itakayotolewa.
Social Plugin